Waziri aibana TANROADS...soma habari kamili na matukio 360..#share
Na Mwandishi Wetu, Njombe
NAIBU Waziri wa Ujenzi,
Elias Kwandikwa, ameuagiza uongozi Wakala wa Barabara (TANROADS), Makao
makuu kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja wanaweka mzani mwingine wa
kuhamishika katika eneo la mzani wa Makambako ili kuweza kutatua
changamoto ya msongamano wa magari katika eneo hilo.
Muonekano wa mzani wa
Makambako, mkoani Njombe, wenye uwezo wa kudhibiti uzito wa magari makubwa
yanayozidi 3500kg (tani 3.50).
Ametoa agizo hilo
mkoani Njombe, mara baada ya kufika katika mzani huo ambapo amejionea
changamoto zake na kusisitiza kuwa, kuongeza mzani wa kuhamishika katika
eneo hilo kutasaidia kupunguza kero hiyo ya msongammano wakati Serikali
ikitafuta ufumbuzi wa kudumu wa kujenga mzani mwengine katika eneo hilo.
"Naagiza TANROADS
Makao makuu mfanye kila linalowezekana ndani ya mwezi mmoja mlete mzani
wa kuhamishika hapa Makambako, tunataka tutoe huduma ya haraka kwa
madereva ili pasiwe na msongamano katika eneo hili",
amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Amewaonya wale madereva
wote wanaotumia kisingizio cha uwepo wa foleni
katika mzani huo kwa kufanya mambo yao binafsi kuacha mara moja tabia
hiyo, kwani ikibainika kwa dereva yeyote ambae ameshapatiwa huduma lakini bado
ameegesha gari lake katika eneo hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria dhidi
yake.
Ameagiza Taasisi zote
zinazotoa huduma katika mzani huo kushirikiana na kuandaa maoni yao kuhusu
namna ya kupunguza msongamano katika mzani huo na kuyawasilisha Wizarani ili
yaweze kufanyiwa kazi.
Kwa upande wake, Meneja
wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Njombe, Mhandisi, Yusuph Mazana,
ametaja baadhi ya changamoto zilizopo katika Mzani huo kuwa ni kuharibika kwa
mzani mara kwa mara kutokana na mzani huo kuwa ni wa siku nyingi na kuwepo na
muingiliano wa huduma kutoka Taasisi mbalimbali za serikali kama
Uhamiaji, Polisi na TRA.
Ameongeza kuwa
changamoto nyingine ni baadhi ya magari kuegeshwa nje ya maeneo ya mzani baada
ya kupima na hivyo kusababisha msongamano wa magari yanayotakiwa kuingia ndani
ya eneo la mzani kwa ajili ya kupata huduma ya upimaji au kufanya taratibu
nyingine.
Naibu Waziri Kwandikwa
amemaliza ziara ya kikazi katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ambapo
alipata fursa ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali
inayotekelezwa na Sekta yake.
No comments:
Post a Comment