AG ataka akaunti kampuni Rifaro Africa LTD izuiwe...soma habari kamili na matukio360...#share
Na Abdulrahim Sadiki Dar es Salaam.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Dk Adelardus Kilangi amewasilisha maombi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akiomba kuzuia akaunti ya kampuni ya upatu ya Rifaro Africa Limited.
Pia anaomba walalamikiwa katika shauri hilo ambao ni wakurugenzi wa kampuni hiyo, Jones Moshi, James Gathonjia na kampuni hiyo wazuiwe kujihusisha na fedha zilizopo katika akaunti namba 3301106013 yenye jina la Rifaro Africa Limited iliyopo katika Benki ya Kenya ' KCB' tawi la Mlimani City.
Dk Adelardus Kilangi
Wanaomba Meneja wa tawi hilo la Benki kutoruhusu ama kuwezesha wahusika kushughulika na akaunti hiyo.
Maombi hayo yamepangwa kusikilizwa mahakamani hapo Machi 7,2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Kwa mujibu wa maombi hayo ambayo yameungwa mkono na kiapo cha Wakili wa Serikali, Shedrack Kimaro ambapo anaeleza kuwa walalamikiwa hao wapo katika uchunguzi wa makosa ya kula njama na kuendesha upatu.
Kesi hiyo inafanyiwa uchunguzi na askari polisi Fadhili Mndem kama kiongozi wa wapelelezi.
Ilidaiwa kuwa mlalamikiwa wa kwanza Jones ni Mfanyabiashara na Mkazi wa Mbezi na kwamba mlalamikiwa wa pili James ni Mfanyabiashara na Mkazi wa Nairobi Kenya na kwa upande wa mlalamikiwa wa tatu ni kampuni imesajiliwa nchini na ofisi zake zipo Kijitonyama.
Iliendelea kudaiwa kuwa baada ya kampuni hiyo kusajiliwa ilipata leseni ya kufanya biashara katika Manispaa ya Kinondoni ya kuuza vocha za simu na vifaa vya simu.
Wakati wa kufanya biashara zake kampuni hiyo inadaiwa kuwa ilianza kuwashawishi wananchi kujiunga na kampuni hiyo kama wasambazaji wa muda wa maongezi na kuendesha semina.
Wanachama walishawishiwa kujiunga kwa kulipa Sh128,500 kama gharama ya usajili ambayo hairudishwi na kwamba fedha hizo zilikuwa zinaingizwa katika kampuni hiyo.
Kwa wanachama waliojiunga wanadaiwa kupewa jukumu la kutafuta wanachama wapya kujiunga na hiyo kampuni na kwa kila mwanachama mpya aliyemtafuta hupata kamisheni ya Sh 20,000.
Anadaiwa kuwa ukifanikiwa kupeleka wanachama wengi zaidi unaweza kushinda gari, nyumba ama kiwanja.
Iliendelea kudaiwa kuwa kwa muonekano wa hiyo biashara ni upatu na kwamba kutokana na ahadi hizo wanachama takribani 12,956 wamejiunga Mara baada ya kulipa kiingilio.
Maombi hayo pia yameungwa mikono na ASP Fadhili Mndem.
Aliongeza kudaiwa kuwa katika wakurugenzi hao, Jones anahisa katika kampuni hiyo 8480, James ana hissa 2880 na Mosses Diffu alikuwa na hissa 2880 ambapo aliziuza kwa Jones.
About Author Matukio360
Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.




No comments:
Post a Comment