WAZIRI: Zanzibar imenufaika na ujio wa FIFA....soma habari kamili na matukio360...#share
Na Mwajuma Kombo, Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema imenufaika na ujio wa ujumbe wa rais wa shirikisho la soka la dunia Fifa Gianni Infantino na matarajio makubwa ni soka ya Zanzibar kupiga hatua kubwa ya maendeleo hadi kiwango cha kimataifa.
Rashid Ali Juma
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari Utangazaji Michezo na Utalii Rashid Ali Juma wakati alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu matunda ya ujumbe wa viongozi wa Shirikisho la soka la Fifa suali lililoulizwa na mwakilishi wa jimbo la Mfenesini Machano Othman Said.
Juma aliyataja baadhi ya matunda yaliyopatikana katika ujio wa ziara ya rais wa Shirikisho la soka Fifa ni makubaliano ya Zanzibar kujengwa viwanja viwili vya soka.
Amesema mikoa 9 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vitajengwa viwanja ambapo Zanzibar vitajengwa viwili ikiwemo Unguja na Pemba.
‘’Hayo ni baadhi ya matunda ya ujio wa rais wa Shirikisho la soka la Dunia Fifa…..Zanzibar itapatiwa viwanja viwili ambavyo vitajengwa kimoja Unguja na chengine Pemba na vyengine 7 kujengwa mikoa ya Tanzania Bara.’’alisema.
Aidha alisema Zanzibar itapatiwa mgao wa jumla ya Dola za kimarekani Laki 100,000 katika mgao utakaopewa chama cha soka nchini TFF ili kuendeleza masuala ya soka na utawala wake.
‘’Hizo dola Laki 100,000 tutakazopewa hivi karibuni kwa mujibu wa ahadi ya rais wa Fifa zitatumika katika kuimarisha soka ya wanawake,soka la ufukweni pamoja na soka la vijana’’alisema.
Aidha alisema katika makubaliano hayo Zanzibar sasa itanufaika na mgao unaotolewa na Fifa kwenda kwa chama cha soka cha Zanzibar ZFA takriban dola za kimarekani Milioni 1,250,000 ambapo Zanzibar itapata dola 250,000.
Alisema ziara ya rais wa Shirikisho la soka Fifa ilikuwa na mafanikio makubwa ambapo shukrani za dhati ziende kwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli ambaye alitoa maelekezo yote yaliyosomwa na Waziri mkuu Kassim Majaliwa ambaye alionana na rais wa Fifa.
Alisema Ujumbe wa Fifa kwa ufupi ulifahamu mfumo wa uendeshaji wa soka katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuelewa kwamba masuala ya soka kila upande unayo mamlaka ya uendeshaji na usimamizi wake isipokuwa katika ngazi ya timu ya taifa.
‘’Mafanikio ya ziara ya rais wa FIFA yanatokana na maelekezo ya rais John Pombe Magufuli ambayo yalisomwa na waziri mkuu ambayo yalifahamika kikamilifu na uongozi wa FIFA na kuahidi mambo mengine kuyafanyia kazi zaidi’’alisema Juma.
Waziri Juma pamoja na Waziri wa Habari Utamaduni na sanaa na michezo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano dkt.Harrison Mwakyembe walishiriki kikamilifu katika mapokezi ya ujumbe wa uongozi wa Fifa katika uwanja wa ndege wa Dar-es-Salaam wiki iliyopita.




No comments:
Post a Comment