Huduma ya afya sasa kutolewa kielektroniki....soma habari kamili na matukio360..#share
Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
WIZARA ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto inatarajia kukusanya na kutumia takwimu kwa njia ya kielektroniki nchini ili kutoa huduma za afya kwa ubora.
Dk Mpoki Ulisubisya
Hayo yameelezwa leo jijini Dar es Salaam na katibu mkuu wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia ,wazee na watoto Dk. Mpoki Ulisubisya wakati wa kuweka sahihi ya makubaliano ya kuanzisha mfumo wa ukusanyaji takwimu za afya utakaotekelezwa na Wizara ya afya,Wadau wa Maendeleo,Asasi za Kiraia na Shirika la Afya Duniani (WHO).
“Takwimu ni muhimu zitamuwezesha mtoa huduma kujua historia ya ugonjwa wa mgonjwa na matibabu aliyopewa awali,kuwapa uwezo utumishi kujua tunahitaji rasilimali watu kwa kiasi gani katika kituo cha Afya,” amesema Dk. Ulisubsya.
Dk. Ulisubisya amesema kwa kuanzia mchakato huo utaanza kwenye mikoa ya Tanga,Kilimanjaro na Manyara na hadi kufikia 2020 utakamilika mikoa yote.
Amesema mfumo wa kujaza takwimu kwenye makaratasi umepitwa na wakati na kadri makaratasi ya takwimu yanapokuwa mengi, makosa ya utoaji huduma yanatokea.
Katika hatua nyingine Dk. Ulisubisya amesema hadi sasa hali ya utoaji chanjo imefikia asilimia 97 na lengo ni kufika asilimia 100 kupitia mfumo huu wa kukusanya takwimu kwa njia ya kielektroniki.
Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dk. Matthieu Kamwa amesema wapo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya katika kutekeleza hilo ili kuweza kuboresha mifumo ya afya nchini.
“Unajua Takwimu ni utajiri hasa katika kutekeleza shughuli za kutoa huduma za afya kwa wananchi hivyo hatuna budi kuunga mkono juhudu za Serikali ya Tanzania katika kufanikisha hili jambo litaturahisishia hata sisi katika kutoa miongozo ya afya,” amesema Dk. Kamwa.
![]() |
C
|
No comments:
Post a Comment