CHADEMA:Kuna njama za kumkamata mgombea ubunge wetu ...soma habari kamili na matukio360..#share

Na Abraham Ntambara, Dar es Salaam


CHAMA cha Chadema kimedai kuna mpango maalum wa kukamatwa kwa mgombea  ubunge wa chama hicho jimbo la Siha, Elvis Mossi na kumuweka mahabusu hadi uchaguzi utakapomalizika.

Pia chama hicho kimeshangazwa na  wakuu wa mikoa na wilaya kujihusisha katika kampeni za uchaguzi wakati Nec iliwaandikia barua  viongozi hao ikiwazuhia kushiriki kwenye kampeni.





Dk Vicent Mashinji

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji amedai taarifa walizonazo ni kuwa mpango huo utaongozwa na mkuu wa wilaya ya Siha, Onesmo Buswilu.



"Taarifa tulizonazo kuna mpango maalum wa kumkamata  na kumuweka mahabusu mgombea wetu wa ubunge jimbo la Siha hadi uchaguzi umalizike. Utaratibiwa na mkuu wa wilaya ya Siha, Onesmo Buswilu,'' amesema Mashiji na kuongeza ''Ajabu nyingine ni kuwa pamoja na Nec kuwapiga marufuku wakuu wa mikoa na wilaya kushiriki katika uchaguzi, viongozi hao wanaendelea kuwanadi wangombea wa chama chao."

"Kwa kuwa NEC  ni chombo huru kihakikishe kinasimamia uchaguzi huu kwa uhuru na haki,'' amesema.


Katika hatua nyingine chama hicho  kimelaani kitendo cha mgombea wao wa udiwani kata ya Guhangaza wilayani Muleba mkoani Kagera, Mchungaji Athanas Makoti kutekwa, kuteswa, kunyanyaswa, kuonewa na kulazimishwa  kujitoa kugombea nafasi hiyo.


Pia kimelaani kitendo cha askari polisi waliokuwepo katika eneo la tukio kushindwa kulichukulia suala hilo kwa umakani unaohitajika.

“Hiki ni kitendo ambacho hakikubaliki, ninaimani hata huku kuumizwa alikonako kwa sasa huenda wangeliwahi huyu mgombea wetu asingeumia kwa kiasi hiki alichoumia kwa hivi sasa,” amesema Dk Mashinji.

Amesema kwa mujibu wa ushuhuda wa mgombea huyo na watu wengine hawana shaka kuwa tukio hilo ni njama za kisiasa zenye uhusiano na uchaguzi wa marudio katika kata ya Guhangaza, wilayni Muleba, mkoani Kagera.

Amesema taarifa walizonazo ni kwamba hospitali aliyokuwa akipatiwa matibabu imempa rufaa akapate matibabu zaidi na kueleza hali hiyo inaonesha  ni kwa kiasi kikubwa   meumizwa.

Dk Mashinji amelitaka jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa haraka dhidi ya kitendo hicho na kutoa taarifa mapema ili  aliyehusika  afikishwe  kwenye vyombo vya sheria.






About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search