Tido Mhando asomewa maelezo ya awali mahakamani ......soma habari kamili na matukio360...#share
Dar es Salaam.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemsomea maelezo ya awali (PH) Mkurugenzi mkuu wa zamani wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando ambaye anayekabiliwa na mashtaka matano ikiwamo matumizi mabaya ya madaraka.
Kabla ya kusomewa maelezo hayo mbele ya Hakimu Mfawidhi, Victoria Nongwa, Tido alikumbushwa mashtaka yanayomkabili na Wakili wa Serikali Dismas Mganyizi.
Tido Mhando akiwa katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu
Katika maelezo hayo ya awali, Tido alikubali maelezo yake binafsi na kwamba alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC mwaka 2006 hadi 2010.
Alikubali kuwa alikuwa msimamizi katika shughuli za TBC lakini siyo kwa shughuli zote.
Pia alikubali kutoka maelezo katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) lakini hakukiri na kuwa alifikishwa mahakamani Januari 26,2018.
Kwa upande wa mashtaka yanayomkabili, Tido aliyakana na kesi itaanza kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka Machi 28,2018.
Tido anakabiliwa na mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh887.1 milioni.
Inadaiwa kuwa Juni 16, 2008 akiwa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Tido ambaye alikuwa mkurugenzi wa TBC, kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila ya kupitisha zabuni, kitu ambacho ni kinyume na Sheria ya Manunuzi na kuinufaisha BVl.
Katika shtaka la pili, Tido anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake Juni 20, 2008 aliposaini makubaliano kwa utangazaji wa digitali duniani kati ya TBC na BVl.
Katika shtaka la tatu, anadaiwa Agosti 11, 2008 na Septemba 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa ununuzi, usambazaji kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.
Katika shtaka la nne, anadaiwa kuwa Novemba 16, 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT Broadcast Infrastructure) kati ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.
Katika shtaka la mwisho, anadaiwa kuwa kati ya Juni 16 na Novemba 16, 2008 akiwa UAE, Tido aliisababishia TBCli hasara ya Sh887,122,219.19.
Tido anatetewa na Wakili Ramadhani Maleta na yupo nje kwa dhamana.
About Author Matukio360
Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.




No comments:
Post a Comment