Vigogo Six Telecoms waendelea kusota rumande.....soma habari kamili na matukio360....#share


Na Abdulrahim Sadiki, Dar es salaam


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka katika
kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wanne wa Kampuni ya Six Telecoms Limited na kampuni yenyewe kukamilisha upelelezi.


Hakimu Mfawidhi,Victoria Nongwa amesema hayo leo baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi Kishenyi Mutalemwa kudai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Kishenyi amedai  wapelelezi katika kesi hiyo wanafanya jitihada za kukamilisha upelelezi  na kwamba upelelezi upo katika hatua nzuri na anaamini muda si mrefu utakamilika.

Kesi imeahirishwa hadi Februari 23,2018 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

Washtakiwa  wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Mhandisi  na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya  Six telecoms,   Hafidhi  Shamte maarufu Rashidi  Shamte, Mfanyabiashara na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Peter Mayunga Noni, Mwanasheria na Mhadhiri na Mkurugenzi wa hiyo kampuni,Ringo Willy Tenga,  Mkuu wa fedha wa kampuni hiyo Noel Odeny Chacha na Kampuni ya Six Telecoms Limited.  

Katika kesi hiyo namba 73 ya 2017, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwamo ya utakatishaji wa fedha ambapo  wanadaiwa   kuwa kati ya Januari 1,  2014 na Januari 14,2016 Dar es Salaam, walitoza maalipo ya Mawasiliano ya simu za kimataifa  chini ya kiwango  cha dola 0.25 kwa  dakika kwa lengo la kujipatia faida.

Katika shtaka la pili, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa  kati ya Januari Mosi ,2014 na Januari 14, 2016 kwa udanganyifu na kwania ya kuepuka maalipo, walishindwa kulipa kiasi cha dola 3,282,741.12 kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kama maalipo ya mapato.

katika shtaka la tatu, inadaiwa kuwa washtakiwa hao katika kipindi hicho cha  kati ya Januari Mosi 2014 na Januari 14, 2016 walishindwa kulipa ada za udhibiti za dola 466,010.07 kwa TCRA.


Katika shtaka la nne la utakatishaji wa fedha, Hafidhi, Noni,Tenga na Chacha wanadaiwa kuwa kati ya Januari 2014 na Januari 14, 2016 walijipatia, walitumia ama walisimamia dola 3,282,741.12 wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya udanganyifu linalotokana Mashtaka yaliyotangulia.

Katika shtaka la tano la utakatishaji fedha, inadaiwa kuwa kampuni ya Six Telecoms Limited kati ya Januari 2014 na Januari 14, 2016  ilijipatia, ilitumia na kusimamia dola 3,282,741.12 wakati ikijua fedha hizo ni zao la makosa ya udanganyifu yanayotokana Mashtaka yaliyotangulia.

Katika shtaka la sita, washtakiwa hao  wanadaiwa kuwa waliisababishia mamlaka hiyo ya TCRA hasara ya dola za kimarekani 3,748,751.22, sawa na Sh 8 bilioni  za kitanzania.



Baada ya kusomewa Mashtaka hayo hawakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu Mahakama hiyo haina Mamlaka hadi Mahakama Kuu. Wapo rumande Kwa sababu mashtaka ya utakatishaji fedha yanayowakabili ni miongoni mwa mashtaka yasiyo na dhamana.



About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search