Atiwa mbaroni kwa kupora, kubaka na kuwapiga wanawake picha za utupu...soma habari kamili na matukio360..#share


Na Mwandishi Wetu, Morogoro

JESHI la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia Mabula Mabula maarufu Six mkazi wa mjini humo,  kwa tuhuma za uporaji wa simu kwa kutumia pikipiki, kubaka na kuwapiga picha za utupu wanawake kisha kuzisambaza mitandaoni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei

Akizungumza leo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Ulrich Matei amesema mtuhumiwa huyo amekamatwa baada ya makachero, kikosi cha kupambana na uhalifu  mitandaoni pamoja na kikosi cha kupambana na ujambazi, kumfuatilia kwa ukaribu.

Akihojiwa mara baada ya kukamatwa, Mabula ameeleza mbinu anazotumia ikiwa ni pamoja na kujifanya askari polisi, kuwakamata wanawake nyakati za usiku, kuwasingizia makosa mbalimbali na kuwapeleka maeneo yenye giza na kuwabaka.

Mtuhumiwa huyo ameyataja maeneo anayofanyia matendo hayo kuwa ni Msamvu Relini na kwamba amekuwa akitumia mapanga kuwatisha wanawake hao na kuwapiga picha za utupu na baadaye kutishia picha hizo kuzituma kwenye mitandao ya kijamii.

“Hizo picha huwa nawapiga kwa kutumia simu zao na anayekataa kunipa hela huwa naondoka na simu yake na kisha natuma hizo picha kwenye mitandao iliyopo kwenye simu hizo, baada ya hapo simu naiuza napata hela,” amesema mtuhumiwa huyo.

Katika  mahojiano na polisi, mtuhumiwa huyo amemtaja mwezake mmoja Ramadhani Salumu maarufu Miondoko mkazi wa Manispaa ya Morogoro kuwa ndio mnunuzi wa simu hizo za wizi.

Katika msako huo polisi wamefanikiwa kumkamata Salumu na kwamba wote watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.


About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search