Chadema yashutumiwa kuingilia uhuru wa mahakama...soma habari kamili na matukio360...#share

Na Abraham Ntambara, Dar es Salaam
WATETEZI wa Rasilimali Wasio na Mipaka (Warami) wamekituhumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuingilia uhuru wa mahakama kwa kuishinikiza kuwapatia dhamana viongozi wake.
Mkurugenzi wa Utafiti Warami Philipo Mwakibinga, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam.
Shutuma hizo zimekuja siku moja baada ya Chadema kufanya mkutano na vyombo vya habari na kuitaka mahakama kutenda haki kwa kuhakikisha inawapatia dhamani viongozi wa chama hicho waliokuwa wamewekwa mahabusu kwa kukabiliwa na kesi za uchochezi na uvunjifu wa amani ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Utafiti Warami Philipo Mwakibinga amesema Godbless Lema, Profesa Abdallah Safari na wenzao wakiwa wanajua kuwa mahakama ni chombo cha haki walitengeneza mazingira ya kuonyesha kuwa viongozi wao hawatendewi haki.
“…ilhali wakijua wazi jambo hilo limelenga kuishawishi na kuilazimisha mahakama ifanye watakavyo wao kwa kuacha misingi ya haki wajibu na maadili ya kimahakama,” amesema.
“Sote ni mashahidi kwamba Mbowe na wenzake wamekamatwa kama matokeo ya matendo yao ya kushawishi na kuchochea chuki miongoni mwa watanzania jambo ambalo si la kiutamaduni kwa Watanzania,” amedai Mwakibinga.
Mwakibinda amewakumbusha watanzania kuwa sheria ni kaa la moto, na unapovunja sheria lazima ujue kuwa umeamua kushika kaa la moto kwa hiyo lazima ujiandae kuungua ambapo amewataka Chadema hususani Leman a wanzao watii sheria na waache maneno ya uchochezi.
Ameitaka Chadema kuiacha mahakama itafsri sheria na kwa kuwa wameweka wanasheria wanaowaamini, wawahimize kujikita kuhakikisha wanashinda kesi zinazowakabili.
Katika hatua nyingine Warami wamesema matukio ya Chadema kuunga mkono waraka wa Maaskofu na ACT-Wazalendo kumfukuza uanachama Mkurugenzi huyo wa Warami kwa kuukosoa waraka huo na Maalim Seif kuunga mkono vinaashiria na kuthibitisha kuwa maaskofu wameamua kutumika.
“Mwisho tunawaasa wanasiasa, wanaharakati, wanahabari, viongozi wa dini, NGO’S na wengineo waanzishe utaratibu wa kuheshimu uhuru wa mahakama na kuto kutoa kauli za mashinikizo,” amesema.
No comments:
Post a Comment