LHRC: Uchaguzi Kinondoni, Siha ulivunja sheria, haki za binadamu...soma habari kamili na matukio360...#share


Na Abraham Ntambara, Dar es Salaam

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimedai uchaguzi mdogo wa marudio ya ubunge katika jimbo la Siha na Kinondoni uligubikwa na ukiukwaji wa haki za binadamu, sheria na taratibu zinazoratibu chaguzi.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga akionesha waandishi wa habari jijini Dar es Salaam nakala ya ripoti ya uchaguzi wa marudio ya ubunge wa Kinondoni na Siha uliofanyika Februari 17, 2018.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga alipokuwa akitoa ripoti ya uchaguzi huo uliofanyika Februari 17, 2018 mbele ya waandishi wa habari.

“Katika kutimiza jukumu hilo la kidemokrasia, LHRC kimefanya uangalizi tangu zilipoanza kampeni mnamo Januari 25, 2018 na wakati wa uchaguzi ambapo katika chaguzi hizo ndogo chama cha Mapinduzi kilishinda. Hata hivyo LHRC kimebaini masuala kadhaa ya ukiukwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa sheria na taratibu zinazoratibu chaguzi kama zilivyoainishwa,” amesema Henga.

Amesema wakati wa kampeni kulishuhudiwa kutumika kwa watoto suala ambalo ni kinyume na kifungu namba 12 cha sheria ya mtoto, 2019 kinachokataza kuwaajiri watoto katika shughuli yoyote ile ambayo ni hatarishi kwa maslahi mapana ya mtoto, kiafya, kielemu kiakili, kimwili pamoja na maendeleo ya kimaadili.

“LHRC kimeshuhudia video ya mtoto mdogo aliyekuwa jukwaani akitumika katika mkutano wa kampeni wa Chama cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika Makumbusho katika jimbo la kinondoni Februali 2, 2018. Huu ni ukiukwaji wa haki za binadamu hususani haki za watoto,” amesema.

Henga ameongeza kuwa kulikuwa na matumizi ya rasilimali za umma kwa maslahi ya vyama ambapo amesema kuwa viongozi wa serikali walitumia magari ya umma katika mikutano ya kisiasa kinyume na sheria ya vyama vya siasa na sheria ya uchaguzi haswa sheria ya gharama za uchaguzi ya mwaka 2010.

Amesema pia kulikuwa na matumizi ya nguvu yaliyopelekea watu kujeruhiwa na kuuawa ambapo ameeleza kuwa matumizi hayo ya nguvu yalitumika kipindi cha kampeni na kupelekea raia kuumizwa na hatimaye vifo. Ametoa mfano kuwa ni kuuawa kwa mwanafunzi wa NIT Akwilina Akwilini aliyeuawa na polisi wakisambaratisha waandamanaji wa Chadema  na kuwashikilia wafuasi 40 wa  chama hicho.

Kipindi cha Uchaguzi
Amesema wakati wa uchaguzi walibani dosari kadhaa zikiwemo,  mwitikio mdogo wa wapiga kura, unyanyasaji wa mawakala wa vyama vya siasa, uwezo mdogo wa wasimamizi wa uchaguzi, mazingira yasiyo rafiki kwa wapiga kura na watu wenye ulemavu.

Nyingine ni uwepo wa mabango ya wagombea katika vituo vya kupigia kura, kutokuwepo kwa usiri katika eneo lakupigia kura, uwepo wa polisi wengi vituoni, kupotea kwa shahada na vituo kutofunguliwa kwa wakati.

Mapendekezo
Kutokana na changamoto hizo LHRC kimetoa mapendekezo kadhaa ikiwa ni pamoja na Tume ya Uchaguzi kutakiwa kuratibu chaguzi mbalimbali kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zilizopo bila kufungamana na itikadi zozote za vyama vya siasa.

Vyama vya siasa hususani chama tawala kuacha kutumia rasilimali za umma hasa katika kipindi cha kampeni na vyama vya siasa kujikita katika kuhubiri Ilani za vyama vyao na kuacha kutumia kejeli, matusi na vijembe katika kampeni.



About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search