Janeth Magufuli atoa neno ..... soma habari kamili na matukio360...#share


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MKE wa rais Mama Janeth Magufuli leo ameongoza maelfu ya wanawake mkoa wa Dar es salaam kuadhimisha kilele cha Siku ya Wanawake Duniani na ameziomba asasi za kiraia, watu binafsi kushirikiana na serikali kutoa mbinu mbalimbali, mafunzo, mitaji na kuwatafutia masoko ya bidhaa wanawake.
Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akijumuika na maelfu ya wanawake wa mkoa wa Dar es salaam kuadhimisha kilele cha Siku ya Wanawake Duniani katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam.

Mama Magufuli pia ameupongeza mkoa wa Dar es salaam kwa kuanzisha vikundi zaidi ya 400 vya wanawake vinavyojishughulisha na shughuli mbali mbali ikiwemo usindikaji mazao, ushonaji, uchoraji na kadhalika, pamoja na kuwa na vikundi vya kukopeshana (VICOBA) vipatavyo 2,748 ambavyo kwa pamoja vina mtaji wa jumla ya shilingi bilioni 10.78.

"Ni imani yangu kuwa kama mikoa yote na taasisi nyingine za kiserikali na kiraia zitaiga mfano wa Dar es salaam katika kuwawezesha wanawake kiuchumi pamoja na kuwashirikisha kwenye shughuli za ujenzi wa viwanda basi tutawawezesha wanawake kiuchumi ikiwemo kushiriki kwenye shughuli za ujenzi wa viwanda", amesema Mama Mafufuli.

Huku akishangiliwa kwa nguvu, Mama Magufuli amesema japokuwa serikali inajitahidi sana kuweka usawa wa jinsia na kuwawezesha wanawake kisiasa, kiuchumi, elimu na afya, serikali peke yake haiwezi kuzimaliza changamoto zote, hivyo ni lazima wananchi wenyewe washiriki katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.

Mama Magufuli amewapongeza viongozi wa awamu zote za nchi, ikiwa ni pamoja na kinamama shupavu wa TANU na ASP na baadaye CCM ambao kwa namna moja ama nyingine wameshiriki katika harakati za kumkomboa mwanamke nchini.

"Kutokana na umuhimu wa siku ya leo naomba nitambue mchango wa Mama Maria Nyerere, Mama Fatma Karume, Bibi Titi Mohamed, Mama Sophia Kawawa, Bi. Hadija Jabir, Bi Johari Yusuf Akida, Mwajuma Koja, Bi. Mtumwa Fikirini na wengineo wengi. Hatuna budi kuwapongeza sana akinamama hawa kwa kupigania haki za wanawake nchini" alisema.

Mama Magufuli ametanabahisha kwamba japokuwa vitendo vya unyanyasaji, dhuluma na ukatili dhidi ya wanawake bado vinaendelea kwenye baadhi ya maeneo nchini, Tanzania  imepiga hatua kubwa na ni  miongoni mwa nchi zinazosifika duniani kwa kulinda na kusimamia haki na maslahi ya wanawake.

"Hivyo basi hatuna budi kuwapongeza wote walioshiriki katika kulinda na kutetea haki na maslahi ya wanawake nchini", alisema, kabla ya kutembelea maonesho ya wajasiriamali kinamama waliopanga bidhaa zao katika kila pembe ya ukumbi huo.

Sherehe hizo zilihudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda pamoja na wakuu wa Wilaya za Kinodnoni na Ilala, Mhe. Kisare Makori na Bi. Sophia Mjema. 

Wengine ni Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Dar es salaam Mama Kate Kamba, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala, Naibu Kamishna wa Magereza Tusekile Mwaisabila pamoja na maafisa  watendaji wa wilaya ya Ubungo.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search