Prof. Mbarawa : Serikali itaendelea kuiwezesha TMA...soma habari kamili na matukio360...#sharfe
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali itaendelea kuiwezesha
Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA) kuwa na vifaa na mitambo ya kisasa ya hali
ya hewa ili kuwezesha huduma bora za utabiri kutolewa kwa wakati na usahihi kwa
manufaa ya taifa.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akifafanua jambo
wakati wa Siku ya Maadhimisho ya Hali ya Hewa Duniani, mkoani Dodoma, kushoto ni
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Atashasta Nditiye, wa pili Kulia
ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA), Dkt. Agness Kijazi na
kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Nchini (TCAA), Hamza
Johari.
Profesa Mbarawa amesema
hayo mjini Dodoma leo wakati Tanzania ikiungana na nchi nyingine duniani
kuadhimisha Siku ya Hali ya hewa, na kusisitiza kuwa kwa sasa TMA imeongeza
imani kwa wananchi kwani imekuwa ikitoa utabiri wa kuaminika kwa sababu ya kuwa vifaa vingi na vya kisasa vya utoaji taarifa.
“Nipende kuwahakikishia
kuwa Serikali itaendelea kuwezesha TMA na kuhakikisha kuwa inatoa utabiri ambao
ni sahihi na wa uhakika kwani kuwepo kwa utabiri sahihi kutawezesha vyombo
husika kuchukua hatua mapema kabla ya madhara makubwa kutokea” amesema Waziri
Prof. Mbarawa.
Waziri Mbarawa
amewataka wananchi kutunza mazingira kwa kuacha kulima kwenye vyanzo vya maji
na kuepuka kuchafua maeneo ya bahari ili kuepusha athari zinazoepukika zikiwemo
uharibifu wa miundombinu ya uchukuzi.
“Niwaombe wananchi wote watunze mazingira
kwani kumekuwa na uharibifu mkubwa wa miundombinu kutokana na shughuli
zinazofanywa na binadamu katika maeneo mbalimbali yasiyotakiwa kulimwa au
kujengwa, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Kwa Upande wake
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi ameishukuru Serikali kwa jitihada
inazozifanya kuwekeza kwenye miundombinu ya hali ya hewa kwa kutoa fedha
kununua vifaa mbalimbali ambavyo vimewezesha mamlaka hiyo kutoa utabiri
uliosahihi kwa zaidi ya asilimia 70.
Dkt Kijazi ameongeza
kuwa kwa sasa taarifa za hali ya hewa hasa kwenye usafiri wa anga zimeimarika
ambapo hutolewa kila baada ya nusu saa na kuwawezesha watumiaji wa usafiri huo
kupata taarifa kabla ya kuanza safari zao.
“Kwa sasa utabiri wa
usafiri wa anga ni wa uhakika mpaka
asilimia 90 na hutolewa kila baada ya nusu saa na marubani hupata taarifa hizo
kwa wakati kabla ya kuanza safari zao, amesema Dkt. Kijazi.
Siku ya Hali ya Hewa
duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 23 Machi ambapo mwaka huu yanaongozwa
na kauli mbinu isemayo “JIWEKE TAYARI NA ZINGATIA TAARIFA ZA HALI YA
HEWA”.
No comments:
Post a Comment