Samia Saluhu awataka wanaCCM waache uoga... soma habari kamili na matukio360....#share


Na Mwajuma Juma, Zanzibar
MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Samia Suluhu Hassan, amesema  woga unaooneshwa na wanaCCM kisiwani Pemba ni dhahiri kuwa viapo wanavyokula vya kukilinda chama havina ukweli na nia thabiti ndani yake.

Samia Saluhu
Samia ambaye ni makamu wa rais amesema hayo katika tawi la CCM Ole wilaya ya Chake Chake, Pemba, mara baada ya kuweka jiwe la msingi la tawi hilo, ikiwa ni sehemu ya zaira yake ya siku tatu kisiwani hapa.

Alisema lazima vijana wa CCM wajenge ujasiri na uthubutu wa kweli na kujiamini katika kukilinda chama na kuongeza idadi ya wanachama wapya kila siku na sio kukaa na kujenga woga ambao hutoa fursa ya wapinzani kushinda kila zinapofanyika chaguzi.

“Nyinyi ndio wale wanaCCM mnaowatenga wenzenu kwa sababu ya kuzungumza na mtu anaefikiriwa kuwa ni wa upinzani, jamani siasa hizo zimekwisha, kuweni jasiri jengeni chama ili kukiletea ushindi,”alisema.

Aidha alisema wapo wanachama wasio na hamasa  na kuonekana kama CCM haipo ndani ya jimbo la Ole pamoja na maeneo mengine kisiwani Pemba.

Hivyo aliwataka wanachama hao kuyatumia  matawi ya chama chao kuongeza idadi ya wanachama wapya ili CCM iendelee kushika hatamu katika chaguzi kuu na ndogo.
Sambamba na hilo aliwataka wanachama wanawake kutekeleza kwa vitendo nyimbo za umoja na mshikamano wanazoziimba na sio kusema kwa mdomo pekee.
Kuhusu ujenzi wa tawi hilo la CCM Ole, alisema anatamani limazike mwishoni mwa mwaka huu ili liweze kutumika kwa ajili ya matayarisho ya uchaguzi mkuu wa 2020 na kuahidi kutoa  mchango wake kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa tawi hilo, ili likamilike kwa wakati.
Mapema akisoma risala ya ujenzi wa tawi hilo, Katibu wa jimbo la Ole, Yakoub Khalfan, alisema hadi kufikia hatua ya ujenzi huo, shilingi milion 7.6 zimetumika huku shilingi milioni 9.5 zinahitajika kukamilisha ujenzi huo.
Samia amemaliza ziara yake ya siku tatu kisiwani hapa ambapo alitembelea hospitali ya Abdulla Mzee Mkoani, uwekaji wa mawe ya msingi tawi la CCM Chumbageni, Ukunjwi, skuli ya Micheweni, ujenzi wa nyumba za Polisi pamoja na skuli ya Ali Khamis Camp.    


About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search