Sirro atuma salamu za pasaka...soma habari kamili na matukio360...#share

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
INSPEKTA Jenerali wa Polisi, Simon
Sirro anawashukuru Wananchi kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa Jeshi la
Polisi jambo ambalo limesaidia kupunguza uhalifu kwa kiasi kikubwa hapa
nchini.
Kiujumla hali ya usalama hapa nchini
ni shwari na matukio makubwa ya uhalifu wa kutumia Silaha yamepungua kwa
kiasi kikubwa na jitihada za kukabiliana na makosa ya usalama barabarani
zinaendelea ili kupunguza ajali zinazosababisha vifo na majeruhi kwa
raia.
Tunapoelekea kipindi hiki cha Sikukuu
ya Pasaka, Jeshi la Polisi katika mikoa yote linawahakikishia wananchi kuwa
limejipanga kikamilifu kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama
kuhakikisha kuwa sikukuu hii inasherekewa kwa amani na utulivu na hakuna
vitendo vyovyote vya uhalifu vitakavyofanyika na pale vitakapojitokeza
vitadhibitiwa kwa haraka.
Ulinzi utaimarishwa kwenye maeneo yote
yakiwemo maeneo ya kuabudia, fukwe, sehemu za starehe na maeneo mengine ambayo
yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu ili kuhakikisha wananchi wote
wanasherekea sikukuu hiyo katika hali ya utulivu.
Wazazi wanatakiwa kuwaangalia watoto
wao na kutowaacha kutembea peke yao bila ya kuwa na uangalizi wa karibu, pia
wamiliki wa kumbi za starehe wanatakiwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za
uendeshaji wa kumbi hizo ikiwemo kutoruhusu disko toto na kujaza watu kupita
kiasi.
Vilevile Jeshi la Polisi
linawatahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia barabara kuwa makini na
kuzingatia Sheria za Usalama barabarani hasa kwa madereva wa magari na pikipiki
kuepuka kujaza watu kupita kiasi, kubeba mishikaki, kwenda mwendo kasi, kutumia
vilevi pamoja na kupiga honi hovyo.
Nawatakia Pasaka njema.
Share
No comments:
Post a Comment