Halmashauri Temeke kinara vitendo vya rushwa...soma habari kamili na matukio360...#share

Na Abraham Ntambara, Dar es Salaam
TAASISI ya Kuzuia n Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa
Temeke, imesema Halmashauri ya Manispaa ya Temeke inaongoza kulalamikiwa kwa
vitendo vya rushwa katika kipindi cha Oktoba 2017 hadi Machi 2018.
Mkuu wa Takukuru mkoa wa Temeke Pilly Mwakasege, akizungumza na waandishi wa habri jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Takukuru
mkoani humo Pilly Mwakasege alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu
utekelezaji wa majukumu yao kwa kipindi hicho.
“Kati ya malalamiko 232 yaliyopokelewa na ofisi ya Takukuru
Temeke kwa kipindi cha Oktoba 2017 hadi Machi 2018, eneo linaloongoza kwa
kulalamikiwa kwa vitendo vya rushwa ni Halmashauri ya Manispaa ya Temeke,
ambapo malalamiko 87 yalipokelewa na kufanyiwa kazi,” amesema Mwakasege.
Mwakasege amesema eneo linalofuatia kwa kulalamikiwa kwa
vitendo hivyo ni sekta binafsi ambapo ofisi imepokea malalamiko 52 ikifuatiwa
na Mahakama 37, polisi 26 na Idara nyingine malalamiko yalipokelewa na
yanaendelea kufanyiwa uchunguzi.
Amesema kutokana na malalamiko hayo wameshafungua majalada ya
uchunguzi 146 ambapo kati ya hayo, majalada 18 yanaendelea na uchunguzi wa kina
na 60 yanaendelea na uchunguzi wa awali ili kubaini makosa ya rushwa na
kuwafikisha watuhumiwa mahakamani watakapothibitika.
Ameongeza kuwa majalada 68 yalifanyiwa uchunguzi wa awali na
kuthibitika kutokuwepo kwa viashiria vya rushwa hivyo yalifungwa.
Mkuu huyo amesema taarifa 86 ambazo zilipokelewa na kuonekana
kuwa zinatokana na wananchi kutoelewa utaratibu wa kiutendaji katika Idara
mbali mbali za serikali, wananchi walishauriwa utaratibu wa kufuata na
kutafutiwa ufumbuzi wa malalamiko yao.
Aidha amesema katika kipindi hicho pia kiasi cha sh.
44,478,901.59 kimeokolewa kutoka sehemu tofauti, ikiwa sh. 15,794,489.59 ni
mishahara hewa katika halmashauri ya manispaa ya Temeke n ash. 1,000,000 ni marejesho
ya malipo kutoka mfuko wa jimbo la Temeke na sh. 27,684,412.02 ni marejesho ya
malipo ambayo hayakufuata utaratibu wa zabuni katika Chuo cha Taasisi ya
Uhasibu Tanzania (TIA).
Ameleza kuwa wameweza kufungua jumla ya kesi sita mpya
mahakamani huku hadi kufukia mwezi Machi 2018 jumla ya mashauri saba
yaliendelea kusikilizwa mahakamani yakiwa katika hatua mbalimbali ambapo kati
ya hayo, Manispaa ya Temeke idara ya afya ni moja.
Mengine ni Idara ya Elimu Manispaa ya Temeke moja,
TRA-Kigamboni moja, Manispaa ya Ilala Idara ya Ustawi wa Jamii moja, Manispaa
ya Kigamboni Idara ya Afya moja, na watu binafsi shauri moja. Vile vile shauri
moja limetolewa maamuzi mahakamani ambapo Takukuru Temeke ilishinda.
Katika kuhakikisha wanadhibiti mianya ya rushwa, Mwakasege
amesema wanalojukumu la kufuatilia matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo,
kufanya uchambuzi wa mifumo (System Analysis) , kufanya vikao/warsha za
kujadili mianya ya rushwa na kuweka maazimio ya kuziba/kupunguza mianya hiyo
pamoja na kufuatilia utekelezaji wa maazimio hayo.
Ameongeza pia wataendelea kutoa elimu ya rushwa kwa umma,
lengo likiwa ni kuwapa wananchi uelewa kuhusu rushwa, haki na wajibu wao katika
kupambana na vitendo hivyo, pamoja na kuelewa mahali na njia ya kuwasilisha
malalamiko yao kuhusu vitendo vya rushwa.
No comments:
Post a Comment