Tanroads singida yaokoa bilioni 30...soma habari kamili na matukio360...#share

Na Mwandishi Wetu,

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandika amewapongeza Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kusimamia vizuri fedha za miradi na kuokoa  zaidi ya bilioni 30 na kutumia fedha hizo kujenga miradi mingine ya zaidi ya Kilomita 30 kwa kiwango cha lami kwenye barabara ya Mkoa wa Singida.
Ametoa pongezi hizo mara baada ya kukagua maendeo ya sehemu ya ujenzi wa barabara ya Njuki-Ilongero-Ngamu yenye  KM 1.5 katika eneo la Mtipa na kusema kuwa Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuanza usanifu wa barabara ya  Singida-Irongelo-Mkungi-Kidarafa KM 73 kwa kiwango cha lami.

“Niwapongeze TANROADS kwa kuweza kujibana na kutumia fedha za ndani kujenga barabara nyingine kwa kiwango cha lami kwa zaidi ya KM 30, hili ni jambo la kujivunia sana kwa taasisi hii” alisema Naibu Waziri Kwandikwa.

Naibu Waziri Kwandikwa amempongeza mkandarasi GNMS Contractor Co. ltd kwa kazi nzuri anayofanya na kuahidi Serikali itaendelea kuwatumia wakandarasi wazawa katika miradi mbali mbali ya ujenzi wa barabara ili kuwainua kiuchumi wazawa.

“Napenda nimpongeze mkandarasi kwa kazi nzuri anayoifanya kwani amekamilisha  KM 1 nukta 5 na yuko kwenye hatua nzuri kwenye KM 1.5 iliyobaki nakupongeza sana na nisisitize kuwa Serikali itaendelea kuwawezesha wakandarasi wazawa kwa kuwapa miradi ili wakuze mtaji na kufikia kufanya miradi mikubwa zaidi’ alisisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.

Akiongea na  wananchi wa eneo la Ifombo, kata ya Tonge, Mkoani Singida Naibu Waziri Kwandikwa amewataka kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kuweka matuta kwenye barabara bila kuwasiliana na taasisi zinazohusika na miundombinu hiyo kwani vitendo hivyo  vinachangia uharibifu wa barabara na kuhatarisha usalama barabarani.

“Nimewakuta hapa mnaweka wenyewe niwaombe mfuate sheria maana Meneja yuko hapa na hajui kama nyinyi mnajenga matuta,barabara hizi kabla hujafanya kitu chochote ni lazima uwasiliane na wahusika ili kuepuka kuchukua hatua kisheria, kwahiyo niwaombe msiendelee na zoezi hili  kwa sasa”alisema Naibu Waziri Kwandikwa.

Kwa upande wake Meneja wa TANROADS Singida. Eng. Leonard Kapongo amesema mpaka sasa kwenye fedha walizookoa kwenye miradi zimeshajenga KM 20 na hivi karibuni watamalizia KM 10 zilizobaki ili kuwezesha barabara za Mkoani kupitika majira yote.

Eng. Kapongo amemuhakikishia Naibu Waziri Kwandikwa kuwa atamsimamia mkandarasi ili utekelezaji wa miradi ukamilike kwa kuzingatia viwango na kwa wakati.

Naye Mkandarasi wa kampuni ya JNM Contractor, Pius Kandege amemuhakikishia Naibu Waziri kuwa atakamilisha mradi huo kwa wakati na kuukabidhi kabla ya miezi sita ambayo wamekubaliana kwenye mkataba.

Ujenzi wa Barabara hiyo ya KM 1.5 umegharimu kiasi cha Takribani shilingi bilioni 1.5 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi sita.



About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search