Serikali kujadili kodi za mizigo kutoka zanzibar...soma habari kamili na matukio360...#share


NA Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinaendelea kujadiana kuhusu namna bora ya kupata ufumbuzi wa kudumu wa kero ya ulipaji kodi ya mizigo kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara.

Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Wingwi, Mhe. Juma Kombo Hamad (CUF)M aliyetaka kujua kama Serikali ipo tayari kuunda Kamati Ndogo ya Bunge kwa ajili ya kushughulikia mfumo wa ulipaji kodi za mizigo kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara.

Katika sawli hilo Mhe. Hamad alieleza kuwa mfumo wa ulipaji kodi za kusafirisha bidhaa kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara umekuwa ukilalamikiwa kwa muda mrefu kwamba unawakwaza na kuvunja harakati za biashara Zanzibar na hivyo kusababisha uchumi wa Zanzibar kushuka.

Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji, alisema kuwa Serikali hizo mbili zinaendelea kujadiliana ili kuona kuwa suala hilo linapatiwa ufumbuzi wa kudumu na kuongeza kuwa Serikali hizo hazijashindwa kutatua changamoto hiyo na hakuna sababu ya kuunda kamati ya kushughulikia suala hilo.

Alisema chimbuko la malamiko hayo linatokana na kuwepo kwa mifumo tofauti ya kutathmini bidhaa kati ya Zanzibar na Tanzania Bara hali inayosababishwa na viwango tofauti vya ushuru wa forodha vinavyopaswa kulipwa kwa bidhaa ya aina moja kutoka nje ya nchi na kusafirishwa kwenda sehemu ya pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dkt. Kijaji alisema kuwa Mfumo wa uthaminishaji bidhaa zote zinazoingia Tanzania Bara unafanyika kwa kutumia mifumo ya TANCIS na Import Export Commodity Database (IECD) inayoratibiwa na kituo cha Huduma za Forodha kilichopo Dar es Salaam, lakini Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitumii mifumo hiyo na kusababisha kuwepo na tofauti ya kodi kati ya Bara na Zanzibar.

“Kutokana na utofauti wa mifumo inayotumika, bidhaa zote za nje zinazoingia Tanzania Bara kupitia Zanzibar hufanyiwa uhakiki licha ya kuwa zimethaminiwa Zazibar, iwapo uthamini wa Tanzania Bara utakuwa sawa na ule uliofanywa Zanzibar hakuna kodi itakayotozwa Tanzania Bara na ikiwa kodi iliyolipwa Zanzibar ni ndogo, Mamlaka ya Mapato hukusanya tofauti ya kodi iliyozidi”, alisema Dkt. Kijaji.

Alisisitiza kuwa utaratibu wa kukusanya tofauti ya kodi kati ya Zanzibar na Bara kwa kutumia mifumo ya TANCIS na IECD haina lengo la kuua biashara Zanzibar, bali hatua hiyo inalenga kuleta usawa wa gharama za kufanya biashara na ushindani hapa nchini.

Aidha Naibu Waziri huyo alisema kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 63 (2) Bunge ni muhimili unaojitegemea na hivyo Serikali haina mamlaka ya kuunda Kamati ndogo ya Bunge kwa ajili ya jambo hilo au jambo lolote



About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search