JK 'aula' Kimataifa: Sasa Kuhudumu Baraza Kuu la Wakimbizi Duniani (WRC) !

Aliyekuwa rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete ameteuliwa kuhudumu katika baraza kuu la wakimbizi duniani WRC, ambalo ni kundi huru la viongozi na wavumbuzi wanaolenga kubuni mbinu mpya za kutatua mizozo ya wakimbizi.
Kulingana na gazeti la The Citizen nchini Tanzania, taarifa kwa vyombo vya habari ilimtaja Bwana Kikwete kuwa mwenyekiti mwenza wa baraza hilo lililopo chini ya uenyekiti wa waziri wa maswala ya kigeni nchini Canada Lloyd Axworthy.
Gazeti hilo limesema kuwa Hina Jinali kutoka Pakistan na Rita Sussmith kutoka Ujerumani watafanya kazi pamoja na bwana Kikwete kama wenyekiti wenza huku Paul Heinbecker akichaguliwa kama naibu huku naye Fen Hamson akihudumu kama mkurugenzi.
Taarifa hiyo imesema kuwa miongoni mwa mengine, baraza hilo litatoa ushauri wa marekebisho na uvumbuzi ili kuimarisha mfumo wote wa wakimbizi duniani.
Baraza hilo litaleta mabadiliko ili kusaidia kuhakikisha kuwa ushirikiano wa kimataifa kwa wakimbizi unaeleweka, unafanyika kwa njia ya usawa na haki, ilisema taarifa hiyo.
Baraza hilo pia litashirikisha madiwani 17 wa mabaraza.
credit: bbcswahili

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search