nEWS: ACT wamshukia Waziri Tizeba,.. wamtaka ang'atuke kwa kushindwa kazi...#share.
CHAMA cha ACT -Wazalendo kimemtaka Waziri wa
Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba kujiuzulu kwa kushindwa
kuwapelekea wakulima wa korosho pembejeo kama alivyoahidi.
Mbali na kumtaka waziri huyo kujiuzulu, pia kimetoa
mapendekezo 14, likiwemo la kuitaka Serikali kufanya haraka kutimiza ahadi yake
ya kufikisha pembejeo ya bure kwa wakulima wa korosho, kwa kuhakikisha
inafikisha kiwango cha pembejeo kinacholingana na mahitaji yaliyoko.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam,
Katibu wa kamati ya Itikadi, Mawasiliano ya Umma na Uenezi wa chama hicho, Ado
Shaibu alisema Serikali iliahidi kupeleka tani 5,000 za sulphur lakini
imepeleka tani 1,500 tu.
“Matokeo yake wafanyabiashara wanauza sulphur hadi kufikia Sh
80,000 kwa mfuko mmoja badala ya Sh30,000,” alisema.
Kufuatia hali hiyo, chama hicho kimeitaka Serikali kufanya uchambuzi
wa kina wa mahitaji halisi ya kila mkulima na kuwa na uhakika wa bejeti yake
ndipo itangaze na kutekeleza mfumo wa sulpher ya bure na isikurupuke tu kwa lengo la kutaka
sifa.
Amebainisha kuwa serikali inapaswa kufungamanisha sekta ya
korosho na hifadhi ya jamii ili kupitia fao la bei kuweza kuweka uimara wa bei
za mazao na pembejeo.
“Fao la bei litalinda ustawi wa wakulima wa korosho na
kuwaepusha na hasara iwapo bei ya korosho ya msimu huu itaanguka tofauti na
msimu uliopita,” alisema,
Amesema kuwa Mei mwaka huu, kwenye kikao cha mwaka cha wadau
wa zao la korosho kilichofanyika mjini Dodoma, Serikali ilitangaza uamuzi wa
kugawa pembejeo bure kwa wakulima wote wa zao la korosho.
Amesema uamuzi huo ulitangazwa na Dk Tizeba mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye
alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo.
Amesema kutangazwa kwa uamuzi huu kuliibua shangwe kubwa kwa
wakulima wa korosho ambao walifurahia kupunguziwa mzigo wa kununua pembejeo.
“Uamuzi huu ulileta matokeo yafuatayo, Mfumo wa Pembejeo ya
ruzuku ulifutwa. Kabla ya mfumo wa kugawa pembejeo bure kutangazwa, kulikuwa na
mfumo wa pembejeo uliokuwa ukiendeshwa na Vyama vya Msingi vya ushirika (Amcos),”
“Vyama hivi vya msingi vya ushirika vilikuwa vinakusanya
fedha kwa wakulima wakati wa mauzo (kiasi cha shilingi 15,000 tu kwa mfuko),
kununua pembejeo nje ya nchi na kugawa kwa wakulima,” alisema Shaibu.
Aidha amesema kabla ya kutangazwa kwa uamuzi huu, vyama vya
msingi vya ushirika (Amcos) vilikuwa vimeshakusanya fedha kwa wakulima na
vinajipanga kununua Salfa nje ya nchi. Kwa uamuzi huo wa serikali, vyama vya
ushirika viliamriwa kuwarudishia wakulima fedha zilizokusanywa kwa sababu
‘Pembejeo ya bure’ ingeletwa.
Na Abraham Ntambara
No comments:
Post a Comment