eXCLUSIVE: Lipumba, Maalim waendelea Kushikana 'Uchawi'....#share


MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba amesema Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad ameshindwa kutekeleza majukumu yake kama kiongozi, huku akimtaka kurejea ofisini kuendelea na majukumu yake.



Wakati Lipumba akisema hayo na kudai kuwa majukumu ya Maalim Seif  yanakaimiwa na Naibu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya, Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho-Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui amesema Maalim Seif hawezi kufanya kazi na Lipumba na kubainisha kuwa sasa wanapambana na Dola si msomi huyo.

Leo wakati akihojiwa na kituo kimoja cha televisheni, Profesa Lipumba alisema bado anamtambua Maalim Seif kama Katibu Mkuu wa chama hicho licha ya utoro wake kazini.
Katika mahojiano yake ya jana, Profesa Lipumba alisema, "Sijamwona Katibu Mkuu tangu Septemba 23 mwaka jana, namkaribisha aje ofisini Buguruni apokee maelekezo kutoka kwa mwenyekiti.”

Mwenyekiti huyo amesisitiza kwamba yeye ni mwenyekiti halali wa CUF kwa mujibu wa ibara ya 117 ya chama hicho ambayo inaeleza taratibu za kiongozi kujiuzulu.

"Ibara ya 117 inatoa mamlaka kwa mkutano mkuu kujadili barua ya kiongozi kisha kuridhia kujiuzulu kwake au laa. Sasa mimi niliandika barua ya kutengua kujiuzulu kabla mkutano mkuu wa chama haujakaa kuijadili barua yangu ya kujiuzulu," alisema.

Profesa Lipumba amesema chama chake kilifuata taratibu zote za kuwavua uanachama wabunge wanane ambao walibainika kukihujumu chama hicho.

Amesisitiza kuwa yuko tayari kumaliza mgogoro unaondelea kwa vikao vya ndani ya chama, hata hivyo anasikitika kwamba hasimu wake hayuko tayari kwa meza ya mazungumzo.

Akijibu hoja za Profesa Lipumba, Mazrui amesema, “Lipumba hatuwezi  kumsikiliza kwa sababu tunajua anayoyafanya ametumwa na mwenye nchi. Hata aseme nini hatumsikilizi. Hivi ni vita kati ya CUF na Dola, si CUF na Lipumba.”

Amesema vita hivyo vinalenga kuua upinzani na tayari wameshajua wanapambana na nini, kubainisha kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) pamoja na Bunge si wajinga bali wanashinikizwa na Ikulu.

“Lipumba apige kelele hadi apasuke na uzuri ni kwamba tumeshamfukuza na si mwenyekiti wetu tena. Kwa sasa tunaangalia jinsi gani ya kufanya kuhakikisha hali inatulia na demokrasia inarejea,” alisema Mazrui.

“Yeye aseme mpaka apasuke sisi hatumsikilizi. Maalim  Seif hawezi kwenda kufanya kazi na Lipumba na huyo anayejiita mwenyekiti pia hawezi kufanya kazi na CUF inayotambulika.”


Na Mwandishi wetu.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search