mAHAKAMANI kISUTU: Wema 'yamkuta mazito', Mkemia Mkuu adai mkojo wake una dawa za kulevya.....#shar


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeelezwa kuwa, chembechembe za mkojo wa msanii maarufu wa filamu nchini Wema Sepetu una dawa za kulevya.


Hayo yamesemwa leo na Mkemia kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Elias Mulima (40), ambaye ni shahidi wa kwanza katika kesi ya matumizi ya dawa za kulevya inayomkabili Wema na wenzake wawili.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula, Mulima amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu , Thomas Simba kuwa Februari 8 mwaka huu, alipokea sampuli ya mkojo wa Wema ambaye alifikishwa kwenye ofisi hizo akiwa na askari wawili, WP Mary na Inspekta Willy.

Amedai kuwa askari hao walieleza kuwa, walifika hapo kwa ajili ya kumpima mtuhumiwa  Wema mkojo, ambapo kabla ya kumfanyia kipimo alimsajili kisha akamakabidhi WP Mary kontena na kumchukua Wema hadi katika choo maalumu kilichopo katika ofisi hizo kwa ajili ya mchakato huo hilo.

"Baada ya kupata chembechembe za mkojo, nilifanya uchunguzi na kugundua kuwa, mkojo wake ulikuwa na chembe chembe za bangi ambapo kitaalamu bangi  inaonekana kwenye mkojo kwa siku 28", alidai shahidi

Ameendelea kueleza kuwa bangi  inakemikali ambayo inasababisha mtumiaji kuwa na ulevi ambao hauwezi kutibika kirahisi na mtumiaji  huharibika akili.

Amebainisha kuwa kabla ya kupokea sampuli ya mkojo, alipokea bahasha kutoka jeshi la polisi iliyopelekwa na Koplo Robert ambayo ndani yake alikuta msokoto na vipande viwili vya bangi ambayo vilipelekwa pale kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu.

Amedai baada ya kuvipima vipande vile vilikuwa na uzito wa gramu 1.08  na baada ya kufanyia uchunguzi majani yale yalioyesha kuwa na rangi ya zambarau  ambayo inaashiria kuwa yale majani ya mmea  wa bangi pamoja na msokoto wa bangi. Aliandika taarifa ya uchunguzi ambayo ilithibitishwa na mkemia mkuu.

Hata hivyo, shahidi hiyo alipotaka kuwasilisha ripoti hizo kama kielelezo mahakamani wakili wa utetezi, Peter Kibatala alipinga kielelezo hicho kupokelewa na kuidai kuwa ripoti haikidhi vigezo vya sheria kwani mshitakiwa yoyote aliyeko chini ya ulinzi kabla ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu ni lazima maombi yangepelekwa kwanza mahakamani lakini polisi hawakufanya hivyo.

Naye wakili Constantine alipinga vikali na kudai kuwa, hakuna kifungu kinachosema kuwa ni lazima kupeleka maombi mahakamani kama mshtakiwa atakubalio kutii sheria.

Kufuatia mabishano makali, Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 4, mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya uamuzi kama kielelezo hicho kipokelewe au la.


Na Mwandishi Wetu

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search