nEWS: ACT- Wazalendo waja na Ujenzi wa Taifa Huru la Kidemokrasia kwa Maendeleo Endelevu...#share
CHAMA cha ACT- Wazalendo kinatarajia kufanya Mkutano Mkuu wa
Kidemokrasia wa Tatu wenye dhima ya “Ujenzi wa Taifa Huru la Kidemokrasia kwa
Maendeleo Endelevu”
Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara,
Msafiri Mtemelwa akizungumza na waandishi wa habari, alisema utafanyika jijini
Mwanza Agosti 26 mwaka huu.
“Maada mbalimbali kwenye maeneo ya Uhuru, Demokrasia na
Maendeleo zitawasilishwa,” alisema Mtemelwa.
Aidha alisema kwa mujibu wa Ibara ya 29(7) ya Katiba ya ACT toleo
la Mwaka 2015, Mkutano Mkuu wa Kidemokrasia ni jukwaa la mjadala kuhusu masuala
mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kwenye nyanja za siasa, uchumi na utamaduni.
Alisema mkutano huo utawaleta pamoja viongozi wa ngazi
mbalimbali na wanachama wa chama hicho kutoka
pande mbalimbali za nchi, wanasiasa wa vyama mbalimbali wa ndani na nje ya
nchi, wanaharakati mbalimbali, wadau wa maendeleo, watetezi wa haki za binadamu
na wananchi wa kawaida wasio wanachama wa vyama vya siasa.
Matemelwa alibainisha kwamba
mbali na wageni wa ndani, wametuma mialiko kwenye vyama na taasisi mbalimbali
za nje ikiwemo vyama vya Die Linke (Ujerumani), The Altenative (Denmark), PIC
Senegal (Senegal), Cyriza (Ugiriki), Labour (Uingereza), na Red Green Alliance
(Denmark).
Aliwakaribisha Watanzania wote kushiriki kwenye mkutano huo mkubwa
wa kihistoria.
Kwa upande mwingine Mtemelwa alisema mkutano huo pia utakuwa jukwaa mahsusi la kupaza sauti kuhusu
kero za makundi mbalimbali kwenye jamii na jinsi ya kuzitatua. Alitaja kuwa ni
pamoja na sekta ya kilimo cha korosho na suala la ajira, rasmi na zisizo rasmi.
Alisema kwenye suala la ajira watazungumzia suala la Sekta ya
Walinzi Binafsi ambayo ilianza kuchanua nchini miaka ya themanini kama sehemu
ya mageuzi ya kiuchumi na kisiasa.
Alieleza hadi sasa, Tanzania inakadiriwa kuwa na walinzi wa
sekta binafsi zaidi ya milioni mbili. Kundi hilo limeachwa kwenye madhila
makubwa bila kuwa na sauti ya utetezi.
Alitaja baadhi ya changamoto za Sekta ya Walinzi Binafsi ni Tanzania
kutokuwa na sheria mahsusi ya sekta hii kama ilivyo kwa nchi nyingine kama nchi
ya Afrika ya Kusini, sekta hii inatambulika kikatiba (Ibara ya 199(3) ya Katiba
ya Afrika ya Kusini) na inayo sheria mahsusi inayoisimamia (The Private
Security Industry Regulations Act, 2001).
Aidha alisema nyingine ni kampuni nyingi kulipa mshahara duni
kwa walinzi ukilinganisha na kazi ngumu wanayofanya. Alibainisha mishahara hiyo
kuwa ni kati ya sh. 70,000 hadi sh. 150,000.
Aidha alisema uchambuzi mpana utafanyika kwenye mkutano huo
wa Kidemokrasia na watahudhuria wadau mbalimbali wa sekta ya ulinzi binafsi
hasa walinzi wenyewe.
No comments:
Post a Comment