CUF Kimewapongeza Wapinzani kususia hafla kuapishwa wabunge wa Lipumba..Chadai wameletwa kuingiza upinzani bandia...#share
CHAMA cha Wananchi (CUF)
upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad umeupongeza
uamuzi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kususia kuapishwa wabunge wapya wa viti maalumu
wa chama hicho.
Wabunge walioapishwa
juzi wanachukua nafasi za wenzao waliofukuzwa uanachama na Profesa Ibrahim
Lipumba ambaye ni mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama
vya siasa.
Akizungumza na
waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Habari,
Uenezi na Uhusiani wa CUF, Mbarala
Maharagande alisema bado wanawatambua wabunge wanane waliovuliwa uanachama na
kupoteza ubunge.
“Wabunge hawa
walioapishwa jana (juzi) wamekubalika
ili kuingiza upinzani bandia ndani ya CUF na upinzani kwa ujumla. Hatutakubali
kutumiwa katika kutengeneza upinzani ‘feki’ wa kisiasa ili kukisaidia CCM kuendelea
kubaki madarakani,” alisema.
Amesema kitendo cha
kuapishwa wabunge hao kimeshusha haiba ya Spika Job Ndugai kuongoza Bunge
ambalo ni mhimili Dola unaopaswa kuwa alama ya uadilifu katika nchi.
Amesisitiza kuwa CUF
kupitia Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, kitaendelea kuwatambua wabunge na
madiwani wawili wanaodaiwa kuvuliwa uanachama, kusisitiza kuwa bado
wanawatambua kama wanachama wao.
Aliyekuwa Mwenyekiti
wa wabunge wa CUF, Riziki Mngwali amesema
anasikitishwa na hujuma zinazofanywa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa,
Tume ya Uchaguzi (NEC) na Bunge ili kuihujumu CUF licha ya kuwa taasisi hizo
zipo kwa ajili ya kusimamia demokrasia nchini.
“Inasikitisha nchi
iliyojengwa kwa mfumo wa kidemokrasia na taasisi hizi zikipewa mamlaka ya
kuisimamia, lakini badala yake ndiyo zinafanya hujuma dhidi ya Chama cha CUF,”
alisema Mngwali.
Wabunge walioapishwa
juzi ni Alfredina Kaigi, Kiza Mayeye, Nuru Bafadhili, Rukia Kassim, Shamsia
Mtamba, Sonia Magogo na Zainab Amir.
Waliovuliwa
uanachama ni Severina Mwijage, Saumu Sakala, Salma Mwassa, Riziki Mngwali,
Raisa Mussa, Miza Haji, Hadija Ally Al-Qassmy na Halima Mohamed.
Na Abraham Ntambara




No comments:
Post a Comment