TRA yaanza rasmi kukusanya kodi kwenye michezo ya kubahatisha...#share
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema
imeanza rasmi kukusanya kodi kwenye michezo ya kubahatisha kama ambavyo
ilikabidhiwa jukumu hilo kuanzia mwezi Julai kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya
mwaka 2017.
Hayo yameelezwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa
Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA Richard Kayombo akizungumza na waandishi
wa habari kuhusu utekelezaji wa jukumu la ukusanyaji wa kodi katika
michezo hiyo kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Aidha ametaja maeneo ambayo TRA inakusanya mapato katika michezo
mbalimbali ya kubahatisha kuwa ni kama Casino, Sport Betting, Slot Machines,
Lottery na kupitia ujumbe mfupi wa simu (SMS) na kusisitiza kuwa kiwango cha
kodi kinatofautiana kati ya mchezo mmoja na mwingine.
“Jukumu hili limetokana na
mabadiliko ya sheria ambayo yapo katika Sheria ya Fedha ya mwaka 2017 ambayo
imetupa mamlaka kamili ya kusimamia zoezi la ukusanyaji wa mapato katika michezo
ya kubahatisha,” ameeleza Kayombo.
Amefafanua kwamba wanaojihusisha na
michezo hiyo katika Casino wanapaswa kuwasilisha TRA asilimia 15 ya mapato
yanayotokana na mchezo huo kwa wiki huku wanaochezesha michezo ya Sport Betting
wakitakiwa kuwasilisha asilimia 6.
Kayombo ameongeza kuwa kwa wale ambao
wanaochezesha michezo hiyo kwa njia ya SMS watatakiwa kuwasilisha asimilia 30,
kwa michezo ya kitaifa (National Lottery) wanatakiwa kuwasilisha asilimia 10 na
michezo ya slot machine wanatakiwa kuwasilisha sh. 32,000 kwa mwezi kwa kila
machine moja.
“Michezo ya kubahatisha ina pande
mbili yaani mchezeshaji na mchezaji hivyo kila mmoja anapaswa kulipa kodi,
ambapo mshindi wa mchezo huo pia anapaswa kulipa asilimia 18 ya mapato yake
ambayo hukatwa na mchezeshaji na kuiwasilisha TRA,” alisema Kayombo.
Aidha Kayombo amesisitiza kuwa TRA
itajikita zaidi katika ukusanyaji wa mapato tu, jukumu la kuratibu na kuendesha
michezo hiyo litabakia kwa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha hapa nchini ambayo
ndiyo yenye mamlaka na wajibu wa kusimamia michezo yote ya kubahatisha.
Amesema TRA inashirikiana na Bodi
ya Michezo hiyo katika kutoa elimu kwa wadau wote wanaohusika na michezo ya
kubahatisha wakiwemo wadhamini, wananchi, vyombo vya habari na wadau wengine.
Na Abraham Ntambara




No comments:
Post a Comment