Bilioni 702 kujenga barabara mikoani....soma habari kamili na matukio360..#share
Na Abraham Ntambara
SERIKALI
imesaini mikataba minne na kampuni nne za ujenzi wa barabara yenye thamani ya
zaidi ya bilioni 702 kwa ujenzi wa kilomita 402.
Tukio hilo kusaini mkataba hiyo limeshughudiwa na Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, Mwakilishi Makazi wa
Benki ya Mandeleo Afrika (ADB), Hellen Minja, wabunge ambao barabara
zitajengwa, wawakilishi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na
wakandarasi walioshinda zabuni.
Akizungumzia utiaji saini huo Waziri Mbarawa amesema fedha hizo
zitatumika katika ujenzi wa barabara kutoka Tabora, Usesula hadi Mpanda Katavi
kilomita 335 na kilomita 67 kutoka Mbinga hadi Mbamba Bay mkoani Ruvuma.
Mbarawa amesema ujenzi wa barabara hizo ni utekelezaji wa ilani
ya CCM na ahadi za rais John Magufuli wakati wa kampeni.
Amesema fedha hizo zimetolewa na ADB ikiwa ni baada ya serikali
kuomba msaada mwaka 2015 ili kuweza kufungua fursa zilizopo katika maeneo
husika kwa miradi.
Waziri ametumia nafasi hiyo kuwataka wakandarasi walioshinda
zabuni kujenga barabara zenye ubora na viwango kwa kuzingatia muda wa ujenzi.
Mbarawa amesema nia ya serikali ni kuona ujenzi wa barabara hiyo
unakamilika kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
"Naomba Tanroads msimamie ujenzi wa barabara yenye ubora
kwani wakandarasi wengi ni wajanja na ikitokea mtu ameharibu asipewe nafasi
kabisa ya ujenzi wa barabara hapa nchini," amesema.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mhandisi Patrick
Mfugale amesema wakandarasi waliopewa kazi wametokana na uchambuzi mkubwa
uliofanyika kati ya wakandarasi 129 waliojitokeza mwaka 2016.
Amesema ili kurahisisha ujenzi wa barabara hizo wamegawa kwa
wakandarasi wanne ambapo barabara ya Usesula hadi Komanga kilomita 108
itajengwa na Kampuni ya Jiangxi Geo-Engineering Group Corporation Limited ya
China kwa gharama ya zaidi ya Sh.Bilioni 158 na itajengwa kwa miezi 36.
"Komanga hadi Kasinde kilomita 108 itajengwa na Mkandarasi
Kampuni ya China Wu Yi Co. Limited kwa zaidi ya sh.billioni 140 na Kasinde hadi
Mpanda kilomita 105 Mkandarasi Kampuni ya China Railway Seventh Group Co.Ltd
kwa sh. Bilioni 133," amesema.
Mfugale amesema barabara ya Mbinga hadi Mbamba Bay kilomita 67
inajengwa na Mkandarasi China Henan International Corporation Group
Co.Ltd (Chico) kwa sh. Bilioni 129.
Amesema Tanroads imejipanga kusimamia ujenzi huo kwa kufuata
viwango vinavyohitajika vya ujenzi wa barabara nchini.
Mwakilishi Mkazi wa ADB, Minja alisema ofisi yake itaendelea
kutoa mchango kwa serikali katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali nchini pale
watakapo hitajika.
Minja amesema matarajio ya ADB nikuona Tanzania inapata
maendeleo kwa haraka na njia rahisi ni kupitia miundombinu.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Azack Kamwele ambaye
barabara ya Tabora hadi Mpanda inapita jimboni kwake alisema ujenzi huo utafungua
fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mhandisi Stella
Manyanya ambaye pia ni Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji amesema
barabara hiyo itakuwa kiungo muhimu kati ya Tanzania, Msumbiji na Malawi.
Amesema Nyasa ina vivutio vingi vya utalii hivyo ujio wa
barabara hizo utakuwa njia rahisi ya kuwafikisha watalii eneo hilo.
No comments:
Post a Comment