Kesi mhasibu Takukuru upelelezi haujakamilika...soma habari kamili na matukio360..#share


Na Abdulrahim Sadiki, Dar es salaam
UPANDE wa jamhuri katika kesi inayomkabili Mhasibu  Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Godfrey Gugai anayedaiwa kuwa na  utajiri wa kutisha kwa kumiliki mali zenye thamani ya bilioni tatu ambazo haziendani na kipato chake, umedai upelelezi haujakamilika.


Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Peter amedai hayo leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, wakati shauri hilo linalomkabili Gugai na wenzake watatu lilipopelekwa kwa kutajwa.

Kutokana na kutokamilika kwa upelelezi huo, Wakili Peter ameomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa.

Hata hivyo, Wakili wa utetezi, Alex Mgongolwa aliomba upande wa jamhuri watoe maelezo ambayo yataeleza lini upelelezi utakamilika ambapo upande wao utajua siku ya kuanza kwa usikilizwaji wa shauri hilo.

Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Serikali Peter alidai kukamilika kwa upelelezi ni hatua, hivyo hawawezi kueleza kwa asilimia ngapi ila bado unaendelea na wako katika hatua nzuri.

Wakili huyo alidai tareje ijayo wataeleza hatua ya upelelezi ilipofikiwa. Baada ya kusikiliza hoja za pande zote husika, Hakimu Simba aliahirisha shauri hilo hadi Januari 2, mwakani kwa kutajwa na washitakiwa walirudishwa mahabusu.

Mbali na Gugai, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasini Katera

Washitakiwa hao wanaokabiliwa na mashitaka 43 yakiwemo 20 ya utakatishaji fedha haramu, kumiliki mali zisizoendana na kipato na kughushi mikataba ya mauziano ya viwanja katika maeneo mbalimbali.
Gugai na wenzake wanasota mahabusu kutokana na kukabiliwa na mashitaka ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.


Katika mashitaka hayo, shitaka la kwanza ni la kumiliki mali ambazo hazina maelezo ambalo linamkabili Gugai  anayedaiwa kati ya Januari 2005 na Desemba 2015, mkoa wa Dar es Salaam, akiwa ofisa wa umma ameajiriwa na TAKUKURU anamiliki mali zenye thamani ya sh. 3,634,961,105.02 ambazo haziendani na kipato chake cha sasa wala cha nyuma cha sh. 852,183,160.46 na alipotakiwa kutoa maelezo alishindwa kuyatoa juu ya mali hizo zilizoko kwenye umiliki wake.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search