Mkuu wa wilaya awapa watendaji wiki moja...soma habari kamili na matukio360..#share
Na mwandishi wetu, Chunya
SERIKALI wilayani Chunya mkoani Mbeya imetoa wiki moja
kwa watendaji wa ngazi za kata na vijiji kuhakikisha wanaondoa mifugo
iliyoingizwa kwenye maeneo ya hifadhi na vyanzo vya maji.
Mkuu wa wilaya ya Chunya, Rehema Madusa
Agizo hilo limetolewa na mkuu wa wilaya hiyo, Rehema
Madusa katika mkutano wake na viongozi wa vijiji na kata uliofanyika kwenye kijiji cha Itumba na kwamba mifugo itakayokamatwa ipigwe mnada kwa mujibu wa sheria za nchi.
"Ninashangazwa mifugo inazidi kuingizwa kila
kukicha na wafugaji kuvamia maeneo ya
hifadhi kwa kuweka makazi na maeneo ya malisho, sasa watendaji
ni jukumu letu kuhakikisha muda uliopangwa hakuna mfugo utakaoonekana katika
hifadhi," amesema.
Madusa amesema mwaka 2016/17 jumla ya Ng'ombe 260,000 zimehakikiwa
na kutengewa maeneo ya malisho lakini bado mifugo imezidi kuingizwa kiholela.
"Migufo ni changamoto kubwa ambayo inachangiwa na
baadhi ya viongozi wa vijiji kuwabeba wafugaji sasa ni lazima mifugo yote
kuondolewa haraka na watakaoshindwa
kutekeleza agizo hilo hatua zitachukuliwa," amesema mkuu huyo wa wilaya.
Diwani wa kata ya Chalangwa, Petro Nelson amesema uondoaji
mifugo unahitaji muda kwa kuwa mifugo
mingi haijahakikiwa na hakuna maeneo yaliyotengwa kwa matumizi bora ya ardhi na
malisho ya mifugo.
"Agizo hili tutatekeleza lakini linahitaji muda
kwani wafugaji ni wakorofi sana na kuwaondoa kwa ghafla tutasababisha vurugu kubwa zitakazochangia
uvunjifu wa amani,"amesema diwani huyo.
Amekiri kuwa mifugo
inaingizwa kiholela katika maeneo ya hifadhi,
misitu na vyanzo vya maji lakini
ameiomba serikali kutoa muda ili elimu itolewe kwa wafugaji kuhusu madhara na
faida.
Hata hivyo mfugaji kutoka kijiji cha Itumbi, Mabula Shija amesema wapo tayari kuondoa mifugo katika maeneo ya
hifadhi na kuomba Serikali kuona namna ya kuwatengea maeneo ya matumizi bora ya
ardhi kwa ajili ya shughuli za malisho ya mifugo.
No comments:
Post a Comment