Ukatili waendelea kusumbua nchini....soma habari kamili na matukio360..#share
Na Abraham Ntambara, Dar es salaam
KIWANGO cha ukatili wa kijinsia nchini na duniani bado ni
kikubwa na kwa mujibu wa taarifa ya afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya
malaria Tanzania ya mwaka 2015/2016 inaonesha kuwa wanawake 4 kati ya 10
wamewahi kukumbana na ukatili wa kimwili tangu wakiwa na umri wa miaka 15.
Kaimu mkurugenzi mtendaji wa TGNP Mtandao Grace Kisetu akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Takwimu hizo zimeelezwa leo jijini Dar es Salaam na mkuu wa
wilaya ya Ubungo Kisari Makoro akizungumza katika maadhimisho ya kampeni ya
siku 16 za kupinga ukatili wa jinsia iliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia nchini (TGNP Mtandao).
“Asilimia 42 ya wanawake waliowahi kulewa wamekutana na
ukatili wa wenza wao ama wa kimwili au ukatili unaohusisha ngono. Hivyo basi
nawaomba watanzania wenzangu katika maeneo yenu pazeni sauti na kufanya kwa
vitendo kupinga masuala ya ukatili wa kijinsia unaowakumba sana wanawake na
watoto,” amesema.
Amesema kuwa athari za ukatili wa kijinsia ni kubwa katika
nyanja za kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na taifa. Hivyo
ametaka kampeni hiyo ilenge kuinua uelewa wa jamii na wadau mbalimbali kuhusu
madharaya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Mkuu huyo wa wilaya pia amewasisitiza maofisa maendeleo ya
jamii na maofisa ustawi wa jamii wa wilaya na kata zote kuweka mipango thabiti
ya kuonesha kwamba wanashirikiana na wananchi, polisi kukomesha vitendo hivyo.
Ameongeza kuwa serikali inatekeleza mpango kazi wa kutokomeza
ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto (2017/18-22) na kurekebisha
sheria mbalimbali ambazo zinakataza kufanya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi mtendaji wa TGNP Mtandao
Grace Kisetu akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji, amesema lengo kubwa
la maadhimisho ya kapmeni hiyo kwa mwaka huu ni kupinga ukatili dhidi ya watoto
kwa kuboresha mazingira yatakayomwezesha mtoto wa kike kupata elimu sawa na
mtoto wa kiume.
Amesema tafiti zinaonesha kuwa ukatili wa kijinsia umekuwa ni
sehemu ya maisha ya wanawake wengi na watoto kwani mmoja kati ya watoto wa kike
watatu na mmoja kati ya watoto wa kiume saba amekumbana na baadhi ya matukio ya
ukatili wa kingono kabla kabla ya kutimiza miaka 18.
“Asilimia 72 ya watoto wa kike wamekabiliwa na ukatili wa
kimwili na kihisia wakati kwa watoto wa kiume ni asilimia 71,” amesema.
Ameongeza kuwa kumekuwa na mila na desturi zinazowaumiza
watoto na wanawake nchini na ni kutokana na takwimu kuonesha wanawake wanaolewa
wadogo takribani miaka mitano mapema zaidi ya wanaume, zaidi ya asilimia 70 ya
wanawake katika baadhi ya jamii wamekeketwa na takribani wanawake na watoto wa
kike milioni 7.9 nchini wamekeketwa.
Amesema katika maadhimisho hayo TGNP Mtandao imelenga
kuhamasisha uboreshaji wa miundo mbinu na vifaa ili kuimarisha usalama wa
watoto wa kike mashuleni.
No comments:
Post a Comment