Kamati Mapinduzi Cup yajitetea..soma habari kamili na matukio360...#share


Na Mwajuma Juma, Zanzibar
KAMATI ya kombe la Mapinduzi imesema mwaka huu idadi ya ushiriki wa mashabiki katika mashindano ya mwaka huu imepungua, tofauti na miaka iliyopita.

Kikosi cha Azam FC kikiwa na rais wa Zanzibar, Dk Alli Mohamed Shein na makamo wa pili wa rais, Balozi Seif Idd mara baada ya kunyakua ubingwa wa Mapinduzi Cup 2018

Hayo yamebainishwa na mwenyekiti wa kamati hiyo, Gulamu Abdallah Rashid alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tathmini ya mashindano hayo yaliyomalizika Januari 13
mwaka huu, na Azam kutwaa ubingwa.

Amesema hali hiyo imetokana na ugumu wa ratiba ambao ulisababisha
kwa siku kuchezwa  mechi tatu.

‘’Mwaka 2018 kulikuwa na ushiriki mdogo wa mashabiki kufika uwanjani
kuangalia mashindano kutokana na ratiba kuwa ngumu kwani ililazimu kwa siku kuchezwa mechi tatu », amesema Gulamu.

Changamoto nyingine  iliyojitokeza katika mashindano hayo ni kuchelewa kuanza kwa mashindano hayo ambayo yaliathiri
mfumo mzima wa kupanga ratiba huku baadhi ya timu zikiingia katika
adhabu hiyo ya kucheza mechi kila siku.

Changamoto nyengine ni mashindano kutokuwa na mfadhili maalum na kutegemea mapato kupitia viingilio vya uwanjani na kwamba
fedha hizo zilitumika kwa mambo mbali mbali ikiwemo kuzigharamia timu pamoja na kuendesha mashindano.

‘’Changamoto zilikuwa nyingi lakini tulifanikiwa kukabiliana nazo na
kufanikiwa kumaliza mashindano hayo pasipo na matatizo," amesema.

Hata hivyo ameema pamoja na kujitokeza kwa changamoto hizo
lakini wamepata mafanikio makubwa ikiwemo kufanikiwa kukamilisha
mashindano hayo na bingwa kupatikana na kukabidhiwa zawadi kama
ambavyo zilivyotangazwa.

Mashindano ya kombe la Mapinduzi yalikuwa yanashirikisha timu 11
ambapo ni mara ya kwanza kwa mashindano hayo kuwa na timu nyingi
ikilinganishwa na miaka yote iliyopita.

Timu zilizokuwa zikishiriki mashindano hayo kwa Tanzania Bara ni
mabingwa Azam FC, Simba, Yanga na Singida na kwa nje ya Tanzania ni
URA ya Uganda na wenyeji walitoa timu za JKU, Zimamoto, Mlendege,
Jamhuri, Taifa ya Jang’onmbe na Mwenge.

Azam FC iliibuka mshindi wa Kombe la Mapinduzi Cup 2018, baada ya kuifunga URA ya Uganda kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 za mchezo bila kufungana. Azam ilishinda kombe hili kwa mara ya pili mfululizo.

Mlinda mlango wa Azam FC, Razak Abalora alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa fainali hiyo ya Mapinduzi Cup kati ya Azam FC na URA FC, Razak alifanikiwa kuokoa mikwaju miwili ya penati.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search