Tido Mhando apandishwa kizimbani, akabiliwa mashtaka matano...soma habari kamili na matukio 360...#share
Na Abdulrahim Sadiki, Dar es salaam
Mkurugenzi wa Azam Media, Tido Mhando amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ikiwamo mashtaka manne ya Matumizi mabaya ya madaraka na moja la kuisababishia Serikali hasara ya sh milioni 887.
Tido Mhando
Mhando alifikishwa mahakamani hapo nyakati za asubuhi na ilipofika saa 5:22 asubuhi aliingizwa katika ukumbi wa mahakama ya wazi kusomewa kesi yake hiyo.
Ilipofika saa 11:44 asubuhi Hakimu Mkazi Mwandamizi,Victoria Nongwa aliingia mahakamani hapo na Tido alipanda kizimbani.
Baada ya Tido kupanda kizimbani, Mwendesha Mashtaka Wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai akishirikiana na Aneth Mavika na Dismas Mganyizi.
Akisoma shtaka la kwanza Swai alidai kuwa Tido Juni 16,2008 katika maeneo ya Dubai,United Arab Emirates(UAE) akiwa mwajiriwa wa TBC kama Mkurugenzi Mkuu kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa makubaliano kwa ajili ya utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 group Corporation ( BV1) bila ya kupitisha zabuni kinyume na sheria ya manunuzi kifungu namba31 na kuisabishia BVl kupata manufaa.
Katika shtaka la pili Tido anadaiwa kuwa Juni 20,2008 katika utekelezaji wa kazi yake alitumia madaraka vibaya kwa kusaini makubaliano ya utangazaji wa digital duniani kati ya TBC na BVl.
Katika shtaka la tatu, Agosti 11,2008 na Septemba 2008 katika maeneo hayo, Tido anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake kwa kusaini mkataba wa makubaliano wa ununuzi, usambazaji kufunga vifaa vya usambazi na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuisababishia BVI kupata faida.
Shtaka la nne, Tido anadaiwa kuwa Novemba 16,2008 akiwa Dubai ,United Arab Emirates alitumia vibaya madaraka yake kwa Kusini mkataba wa makubaliano(kuongea wakuu wa mkataba ) kwa kuendesha miundombinu ya utangazaji ( DTT broadcast infrastructure) kati ya TBC na BVI na kusababisha BVI kupata manufaa.
Katika shtaka la tano Tido anadaiwa kuwa kati ya Juni 16 na Novemba 16,2008 katika maeneo hayo ya United Arab Emirates aliisababishia hasara TBC ya Sh 887, 122,219.19.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo,Tido ambaye anatetewa na wakili Ramadhani Maleta alikana mashtaka yote.
Swai alidai mahakamani hapo kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Hakimu Nongwa alimtaka mshtakiwa hiyo kutoka fedha taslimu mahakamani hapo Sh 444 milioni ama hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.
Mbali na sharti hilo, pia awe na wadhamini wawili ambapo watasaini hati ya dhamana ya maneno yenye thamani ya Sh 500 milioni na asitoke nje ya nchi bila ya kuwa na kibali cha mahakama.
Mshtakiwa alikamilisha masharti hayo kwa kuwasilisha hati za mali na wadhamini wawili nyakati za saa sita mchana na kuondoka.
Kesi imeahirishwa hadi Februari 23,2018 kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali (PH).
About Author Matukio360
Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.
No comments:
Post a Comment