Chadema walituhumu jeshi la polisi..... soma habari kamili na matukio360...#share

Na Abraham Ntambara, Dar es Salaam

CHAMA cha Chadema kimelituhumu Jeshi la Polisi, ikidai jeshi hilo lililenga kuwashambulia kwa risasi viongozi wa chama hicho.
Kulia ni Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema John Mrema, Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo Banson Kigaila na Ofisa Habara wa Chadema Tumain Makene wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.

Pia kimemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk. Mwigulu Nchemba na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Simon Sirro wajiuzulu kutokana na shambulio hilo.

Shutuma hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Chadema Benson Kigaila alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kudai jeshi hilo limejeruhi raia na kusababisha kifo cha mwanafunzi wa chuo cha NIT walipokuwa wakiandamana kuelekea kwa mkurugenzi wa Kinondoni.

“Tunasema shambulizi hili la risasi lilikuwa linawalenga viongozi wetu, ukiacha mwanafunzi Akwilina Akwilini aliyefariki kwa kupigwa risasi, wengine waliojeruhiwa ni walinzi wa viongozi wetu, kwa hiyo lazima tusema kwamba walikuwa wanalenga viongozi,” amesema Kigaila.

Amesema walinzi hao walishambuliwa sehemu za  nyonga na mapajani na kuwataja kuwa ni Erick John aliyepigwa risasi katika paja la mguu wa kulia na amelazwa katika hospitali ya Mwananyamala.

Wengine ni Innocent Mushi aliyejeruhiwa  kwenye nyonga na kupelekwa hospitali ya Mwananyama kupewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)  yupo hadi sasa, na Rukia ambaye alipelekwa Mwananyamala lakini ndugu zake walimhamisha.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa chama hicho John Mrema amesema  jeshi kushambulia raia, kuwajeruhi na kuua wasilichukulie kama ni suala dogo.

“Tunataka serikali ichukue hatua kwa wale wote waliohusika na mauaji haya, hatujui hadi sasa Mwigulu na IGP wapo ofisini, kama kweli wameguswa na mauaji haya wajiuzulu,” amesema Mrema.

Katika hatua nyingine wameshangaa kauli ya Katibu wa Itikani na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Humphrey Polepole ya kudai kuwa waliosababisha mauaji hayo ni Chadema kwa kufanya maandamano na kulitaka Jeshi la Polisi kumkamata mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe na kumchukulia hatua.

Mrama amedai  kauli hiyo imewashtua na ni ya ajabu na si ya kiuongozi.


“Tunaliomba jeshi la polisi likamhoji Polepole huenda analijua vizuri tukio hili, lakini niwaambie CCM suala hili la kuteka  kuuawa halitaishia kwa Chadema bali litaenda hadi kwa wana CCM,” amesema Mrema.









About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search