Magufuli: Ninawafuatilia majaji wanaokula raha nje ya nchi.....soma habari kamili na matukio360...#share


Na mwandishi wetu, Dar es salaam
RAIS John Magufuli ametoa ya moyoni kuwa anafuatilia mienendo ya baadhi majaji na ameitaka Takukuru, jeshi la Polisi na Magereza kuhakikisha wanawafukuza watendaji wasio waadilifu kwa maslahi ya umma

Pia amesema atahakikisha anakomesha uzembe wa makusudi unaofanywa na wanasheria wa serikali katika kesi mbalimbali inayokabilina nazo na kushindwa na kwamba  Februari hii majibu ya suala hilo yatapatikana.

Rais John Magufuli


Amesema hayo leo jijini Dar es salaam kwenye maadhimisho ya wiki ya sheria nchini na kwamba usheleweshwaji wa kesi bado ni tatizo.

"Wengi wa majaji wanaomba vibali kwa ajili ya  likizo kwenda nje ya nchi ikiwamo Afrika Kusini na Ulaya na wanakaa kwa siku 28 hadi 30. Ninafuatilia kwa makini ili nijue wanatoa wapi fedha za kugharamia safari hizo kwa kuwa mishahara yao ninaifahamu,’’ amesema na kuongeza ‘’Polisi na Mahakama zijiulize kwa nini zinaongoza kwa vitendo vya rushwa kulingana na utafiti wa Twaweza.’’

Amesema suala  la majaji hao ameshamuuliza jaji mkuu, Profesa Ibrahim Juma  lakini hata yeye alikosa majibu sahihi ya kumjibu.

Rais amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika  sekta ya sheria  lakini uadilifu umepungua kwa watumishi wachache wa mahakama, Polisi, Takukuru na kuwa  hawapaswi kuwachwa kwa kuwa ndio wanaodai rushwa wanabambikiza kesi wananchi, na kutoa hukumu kwa upendeleo.

Amesema kupitia tume ya utumishi wa mahakama, mahakimu 27 wamestaafishwa kwa manufaa ya umma kutokana na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma mbalimbali japo walishinda kesi zao  na mahakimu wengine 14 na watumishi 67  wa mahakama wamefukuzwa kazi.

"Polisi, Takukuru, Magereza igeni mfano wa jaji mkuu kwa kustaafisha watendaji wasiokuwa na uadilifu, nilitarajia nanyi mngekuja na majina ya mliowafukuza kazi kutokana na kukosa uadilifu,’’ amesema

Kuhusu serikali kushindwa kesi mbalimbali  rais amesema serikali inashindwa mashauri yake kutokana na ‘weekness’ kutoka ofisi ya mwendesha mashtaka wa serikali (DPP) na kwamba watendaji wazuri wanapelekwa katika ofisi yake (Ikulu) na kwamba kabla ya mwezi Februari kumalizika atatatua changamoto hiyo.

Akitolea mfano rais Magufuli amesema jumla ya kesi 139  zinazohusiana  kodi za kuanzia mwaka 2009 hadi 2015  zenye thamani  bilioni 169.1  hadia sasa hazijapatiwa ufumbuzi.

"Lakini  zingepatiwa ufumbuzi uenda serikali ingeshinda baadhi ya kesi na  ingepata fedha,’’ amesema

Pamoja na mambo mengine ameagiza mapungufu yaliyojitokeza katika sekta ya sheria  yaweze kutafutiwa ufumbuzi na ndio lengo lake la kukubali mfumo wa kisasa wa uendeshaji kesi kwa njia ya  Tehama kwa kuwa itaongeza kasi ya utoaji haki, kudhibiti uzembe na kupunguza gharama za uendeshaji  katika mahakama.

Kuhusu jeshi la Magereza amelitaka  kujitegemea kwa  kubuni mbinu mbadala  ikiwamo kuwatumia wafungwa kuzalisha na kuwabadilisha tabia.

"Jeshi la Magereza lianze kujitegemea sasa kwa kuwatumia wafungwa kwa kuwafanyisha kazi zenye tija na kwamba wafungwa wajifunze vizuri ili wabadilike wanapotoka,’’ amesema

Katika hatua nyingine rais Magufuli amesema anajitathmini  kuhusu utendaji wa watendaji anaowateua.

Amesema hatua hiyo ni kutokana na baadhi ya watendaji serikalini wanakwamisha baadhi ya mambo ikiwamo kuchelewesha kanuni za sheria kwa takribani miezi tisa tangu asaini sheria.

"Nitajitathimini kuhusu watendaji ninaowateua na kwamba kanuni za sheria zimekaa kwa takribani miezi tisa hivyo ninakuagiza waziri wa katiba na  sheria, Profesa  Kabudi katika mwezi huu wa Februari ziwe zimekamilika.’’


About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search