Mkuu wilaya aagiza wanaouza vizimba kariakoo wakamatwe....soma habari kamili na matukio360....#share

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam


MKUU wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es salaam, Sophia Mjema amemtaka Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam(RPC), Razaro Mambosasa kuwakamata wanaouza eneo la vizimba vya kufanyia biashara katika mitaa ya Kariakoo.

Pia wafanyabiashara 1984 kati ya 6140 katika soko la kariakoo wamepewa vitambulisho vya taifa lengo likiwa ni kutambuliwa na serikali na kupata mikopo.

Mkuu wa wilaya ya Ilala, Sophia Mjema akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara katika mtaa wa Kongo Kariakoo jijini Dar es salaam leo




Ametoa agizo hilo leo jijini Dar es Salaam akizungumza na wafanyabiashara (wamachinga) na kutoa vitambulisho vya taifa kwa wafanyabiashara Kariakoo.


Mjema amesema anataka wafanyabiashara wa wilayani humo kuwa mfano wa kuigwa kwa wilaya zingine na kupata mikopo benki zote na hata kusafiri kufuata biashara nje.


"Mitaa haiuzwi, narudia tena mitaa haiuzwi mitaa hii ya serikali... barabara zimejengwa na serikali, wewe unauza ni nani, "amesema.


Amefafanua kuwa wapo wanaouza  vizimba hivyo kwa wafanyabiashara kuanzia sh 500,000 hadi 800,000 na kwamba RPC awakamate watakaofanya hivyo.


Amesema wafanyabiashara hao wanafedha ndogo na  waliochukua fedha za vizimba hivyo kurudisha.


Amesema anafahamu kuwepo kwa viongozi wa serikali wanaochukua fedha kwa ajili ya maegesho ya magari sokoni hapo na kumtaka Katibu Tawala Wilaya Ilala, Edward Mpogolo kuwatafuta na kuchukuliwa hatua.


"Hawa lazima tuwachukulie hatua, tunataka kariakoo iliyo nzuri yenye maadili watu wafanye kazi zao na sisi serikali tupate cha kwetu, "amesema.


Baadhi ya vizimba vya kufanyia biashara katika mtaa ya Kariakoo jijini Dar es salaam

Mjema amesema wafanyabiashara wanapaswa kutoa manung'uniko yao kwa Ofisa Ushirika, Dornad Kivute kuyatatua ili kuwaletea maendeleo na ikishindikana wafike ngazi za juu.

Mwenyekiti wa wafanyabishara hao, Stephen Lusinde amesema kariakoo inawafanyabiashara zaidi ya 6000 na kwamba kuna mitaa 4 iliyorasimishwa kwa ajili ya kufanya biashara.


"Tukio hili ni la kihistoria tangu tupate uhuru haijawahi kutokea, tunaishukuru Serikali ya Rais John Magufuli na Mkuu wa Wilaya, Mjema kwa kutujali sisi wafanyabiashara, "amesema.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search