Morgan Tsvangirai wa Zimbabwe yupo 'mahututi'......soma habari kamili na matukio360...#share
Na mashirika ya kimataifa
Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai yuko hali mahututi katika hospitali moja nchini Afrika Kusini.
Morgan Tsvangirai
Vyombo vya habari vimenukuu vyanzo katika familia yake vilivyosema kuwa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 65 ambaye anatibiwa saratani ya tumbo anakabiliwa na upungufu wa uzani , kuchoka na mishipa yake ya damu kuwa membamba.
Wakati wa harakati zake dhidi ya aliyekuwa rais wa Zimbabwe Robert Mugabe , amepigwa na kufungwa jela mara kadhaa.
Tsvangirai ndiye kiongozi wa chama cha upinzani cha MDC nchini Zimbabwe.
Amekuwa akipelekwa hospitali mara kwa mara tangu mwezi Juni, akipokea tiba katika hospitali moja ya saratani mjini Johannesburg.
Alirejea hospitalini humo mwezi uliopita.
Afya ya Tsvangirai ilidhoofika kwa haraka siku ya Jumatatu , kulingana na duru za familia zilizozungumza na mtandao wa Bulawayo24 siku ya Jumanne.
Alipoteza hamu ya kula na akawa na tatizo kubwa la kula ama hata kumeza maji, duru zilisema.
Tsvangirai pia ameripotiwa kuwa na tatizo la kupumua.
Wakati huohuo Duru za MDC zimesema kuwa Tsvangirai yuko hali mahututi na kwamba watu wanafaa kutarajia lolote lile.
Hata hivyo msemaji wa Tsvangirai, Luke Tamborinyoka alisema kuwa kiongozi huyo wa MDC yuko hali nzuri lakini taifa linafaa kumuombea.
Hospitali ambayo Tsvangirai anatibiwa haijatoa tamko lolote kuhusu swala hilo.
No comments:
Post a Comment