NEC: Jitokezeni kupiga kura....soma habari kamili na matukio360...#share
Waandishi wa NEC, Siha
TUME ya uchaguzi (NEC) leo imewataka watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura, kurejea nyumba na kuendelea na majukumu mengine
Leo wakazi wa jimbo la Kinondoni jijini Dar es salaam na Siha mkoani Kilimanjaro na kata nane watachagua viongozi wao.
Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo Bwana Masani Mashauri akitoa mafunzo kwa Wasimamizi wa Vituo vya Kupigia Kura na Wasaidizi wao kujiandaa na Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Siha na Kata za Kashashi, Gararagua na Donyomuruaki katika Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.
Wakati wito huo ukitolewa, mjumbe wa NEC, Jaji Mstaafu Mary Longway amewataka Wasimamizi wa Vituo vya Kupigia Kura kuzingatia weledi wakati akifungua mafumzo kwa wasimamizi hao.
Jaji Mstaafu Longway aliwakumbusha wasimamizi hao kuwa wanaiwakilisha NEC katika kusimamia vituo, hivyo wakazingatie weledi katika kutekeleza jukumu hilo ili waiwakilishe vyema NEC kwani wakiharibu uchaguzi huo lawama kwa Tume itawarudia wao.
Naye Mkurugenzi wa Habari na Elimu ya Mpiga Kura Giveness Aswile aliwakumbusha wasimamizi hao kwamba msimamizi wa kituo cha kupigia kura ndiye mwenye jukumu la kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki, amani na usalama.
“Kinachokwenda mahakamani wakati wa kesi za uchaguzi ni fomu za uchaguzi kwani zipo kisheria, kwa hiyo mziangalie kwa makini” alisema Mkurugenzi Aswile na kufafanua kuwa:
“Fomu namba 18 ndiyo inayomruhusu wakala wa chama cha siasa kupiga kura nje ya kituo alichojiandikisha na wakati mwingine wakala anatoka Mbeya au Mwanza anakuja Sanya Juu anasema nitapiga kura kwa kutumia fomu hiyo, kwa hiyo kuweni nalo makini.”
Naye Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo la Siha, Masani Mashauri, alisema mafunzo kwa wasimamizi wa vituo wasimamizi wasaidizi na makarani waongozaji yamefanyika kwa ufanisi.
“Lengo kubwa la mafunzo haya ni kuwakumbusha wasiamizi wa vituo kuhusu taratibu za uchaguzi kuanzia hatua ya mwanzo hadi hatua ya mwisho” alisema Mashauri na kuongeza kuwa:
“Nikiwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi wa Jimbo nimefurahi kwamba kazi niliyotumwa na Tume imekamilika kwa ufanisi na wapokeaji wameipokea vizuri elimu hiyo na nina uhakika kwamba kazi wataifanya vizuri kwa mujibu wa Sheria na Kanuni”
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema mafunzo hayo yamekwenda vizuri kwa sababu mambo mengi ambayo walikuwa hawayafahamu wameyaelewa kwa ufasaha.
“Mimi naahidi kufanya kazi kusimamia vizuri uchaguzi ili mwisho wa siku matokeo yawe mazuri yasiyokuwa na utata” alisema mshiriki Wahida Salim Msenga.
Naye Mbaraka Kiure alisema wamejifunza mambo yote yanayohusu upigaji kura na wanaahidi kutenda haki katika kutekeleza majukumu yao kwa kufuata Sheria na Kanuni za Uchaguzi.
Jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro ni miongoni mwa majimbo mawili yanayofanya Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Madiwani na Jimbo lingine ni Kinondoni la mkoa wa Dar es Salaam na kata tano zilizoko katika halmashauri tano za Tanzania Bara huku kata mbili za Manzase na Kimagai wagombea wake wakipita bila kupigwa.
No comments:
Post a Comment