Ulinzi waimarishwa hukumu kesi ya Sugu, Masonga... soma habari kamili na matukio360...#share

Na mwandishi wetu, Mbeya

WAKATI hii leo  hukumu ikisubiriwa, ulinzi umezidi kuimarishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya ambako itatolewa hukumu ya kesi inayomkabili mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi 'Sugu' na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga.

Wakili Peter Kibatala (wakwanza kulia) mwanasheria nguli Profesa Abdallah Safari(Katikati) wakitoa maelekezo kwa Sugu na Masonga mapema walipofika mahakamani

Katika eneo la mahakama wapo askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiimarisha ulinzi nje ya jengo. Tayari washtakiwa wameshafika mahakamani.

Mahakama leo Februari 26,2018 inatoa hukumu ya kesi ambayo Sugu na Masonga wanashtakiwa kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.

Wawili hao wanadaiwa kutenda kosa hilo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Desemba 30,2017 eneo la Uwanja wa Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.

Hukumu inatarajiwa kutolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Michael Mteite aliyesikiliza kesi hiyo. Upande wa mashtaka na wa utetezi ulikamilisha ushahidi Februari 9,2018.

Jamhuri iliwasilisha mashahidi watano na kielelezo kimoja cha sauti iliyodaiwa kurekodiwa na shahidi wa tano, Inspekta Joram Magova.

Upande wa utetezi uliwasilisha mashahidi sita wakiwamo Sugu na Masonga waliokana kutamka maneno wanayoshtakiwa kuyatoa.
Washtakiwa walitetewa na mawakili Sabina Yongo, Boniface Mwabukusi na Hekima Mwasipu kabla ya kujitoa, hivyo sasa wanawakilishwa na Peter Kibatala.

Kwa mara ya kwanza, Sugu na Masonga  walifikishwa mahakamani Januari 16 na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph Pande aliyeeleza upelelezi ulikuwa umekamilika na walikuwa tayari kuendelea na usikilizaji

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search