Wabunge CUF wamwandikia barua rais wa FIFA....soma habari kamili na matukio360...#share
Na Abraham Ntambara,
Dar es Salaam
WABUNGE wa Chama cha
Wananchi CUF wamemuandikia barua ya wazi Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Duniani (FIFA) Gianni Infantino, kumwelezea kilio cha Wazanzibar kuhitaji haki
yao ya Zanzibar kuwa mwanachama FIFA.
Mnadhimu wa Kambi ya CUF Bungeni Ally Saleh akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Pia wamesema watafungua
shauri mahakamani ili kutafuta uhalali wa kikatiba wa chombo cha Shirikisho la
Mpira wa Miguu nchini (TFF) kufanya kazi ya muungano na iizuie TFF kufanya kazi
yoyote mpaka uamuzi utakapotolewa.
Hayo yameelezwa na
Mnadhimu wa Kambi ya CUF Bungeni ambaye pia ni Mbunge wa Malindi, Zanzibar Ally Saleh alipokuwa akizungumza na waandishi
wa habari leo jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuufahamisha umma juu ya barua waliyoandika kwenda kwa rais huyo wa FIFA.
“Sisi wabunge wa
wananchi tunathamini juhudi zinazochukuliwa na kuipigania Zanzibar, lakini kuna
msemo wa Kiswahili unaeleza ukibebwa ujikaze na pia mwengine unaosema mshike
mshike na mwenyewe uko nyuma,”
“Kwa sababu hiyo basi
pamoja na mazungumzo ambayo yatafanywa kuendelea kuishawishi FIFA ielewe hali
ya Zanzibar basi na sisi tumeona pia tupaze sauti zetu hasa kwa sababu viongozi
wa FIFA wapo nchini lakini zaidi kwa sababu rais wa taasisi hiyo yupo nchini,
hivyo tumemwandikia barua ya wazi,” amesema na kuongeza Saleh.
Saleh amesema katika
barua hiyo wamemweleza mambo siti, mambo hayo ni TFF haiwakilishi maslahi ya Zanzibar,
mamlaka ya TFF haijawahi wala hayafiki Zanzibar, muundo wa TFF ni kuwa na vyama
vya mikoa, wakati ZFA ina mikoa yake.
Mengine ni TFF
haijawahi kuwa na sera ya maendeleo inayohusisha Zanzibar, TFF inasimamia
Kilimanjaro Stars na kuifanya timu ya Taifa Stars na mwisho hakuna kikao
chochote cha kikatiba baina ya TFF na ZFA.
Amesema pamoja na
kwenda mahakamani kutafuta uhalali wa TFF kufanya kazi ya muungano, ametaja mambo
mengine watakayotaka kupatiwa ufafanuzi na mahakama ili waweze kufanikiwa
kupata haki yao ya uanachama wa FIFA.
Ametaja kuwa ni kuitaka
mahakama iwape muongozo juu ya kwa nini pasiwepo chama cha soka cha Tanzania
Bara na kutafuta tafsiri ya waziri wa
michezo wa Tanzania Bara kutumika kama ni waziri wa muungano ndani na nje ya
nchi.
Pamoja na hayo
amebeinisha kuwa watatoa hoja binafsi bungeni kuhusu mustakabali ya michezo
chini ya utaratibu tata uliopo hivi sasa.
“Tunaamini bila kufanya
hatua hiyo hapatakuwa na suluhu kwa sababu hali hii imeendelea kwa muda mrefu
na tumekuwa tukijificha kama mbuni kufanya kana kwamba sababu ya Zanzibar
kukosa uanachama wa FIFA haitokani na muungano na muundo wake,” ameeleza Saleh.




No comments:
Post a Comment