Salamba mchezaji bora VPL mwezi Machi...soma habari kamili na matukio360...#share
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Adam Salamba mshambuliaji wa Lipuli ya Iringa, amechaguliwa
kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Machi wa Ligi Kuu ya Vodacom
(VPL)Tanzania Bara.
Salamba ametwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Salum
Kimenya wa Prisons na kipa wa Azam, Mwadini Ally katika uchambuzi uliofanywa
wiki hii na Kamati ya Tuzo hizo.
Kwa mwezi Machi mshambuliaji huyo alionesha uwezo mkubwa na kuisaidia
timu yake kupata mafanikio akifunga mabao matatu kwa dakika 270 alizocheza, ambapo
Lipuli ilicheza michezo mitatu ikishinda miwili na kutoka sare mmoja na kupanda
kwa nafasi moja kutoka ya nane hadi ya saba kwa mwezi huo.
Kwa upande wa Kimenya alicheza dakika 269 na kufunga mabao mawili,
akiiwezesha Prisons kushinda michezo miwili kati ya mitatu iliyocheza na kutoka
sare mmoja, ikipanda kutoka nafasi ya tano hadi ya nne.
Mwadini yeye alicheza dakika zote 270 ambazo timu yake ilicheza kwa mwezi
Machi, ikishinda michezo yote mitatu iliyocheza, ikibaki katika nafasi yake ya
tatu.
Kutokana na ushindi huo, Salamba atazawadiwa tuzo, kisimbusi cha Azam na
fedha taslimu sh. Milioni Moja kutoka kwa wadhamini Vodacom.
Wachezaji wengine ambao tayari wameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi
wa VPL msimu huu na miezi yao katika mabano ni mshambuliaji wa Simba, Emmanuel
Okwi (Agosti), beki wa Singida United, Shafiq Batambuze (Septemba) na
mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa (Oktoba).
Wengine ni kiungo wa Singida United, Mudathir Yahya (Novemba),
mshambuliaji wa Mbao FC ya Mwanza, Habibu Kiyombo (Desemba), mshambuliaji wa
Simba, John Bocco (Januari) na kiungo wa Yanga, Papy Tshishimbi (Februari).
Tuzo za Mchezo Bora wa jumla wa Ligi Kuu Tanzania Bara zinatarajiwa
kufanyika baadaye mwaka huu katika tarehe itakayotangazwa, ambapo licha ya
Mchezaji Bora, pia kutakuwa na tuzo nyingine tofauti kwa kategori mbalimbali.
Share




No comments:
Post a Comment