Chuo Kikuu Huria charejesha rasmi programu ya maandalizi...soma habari kamili na matukio360...#share

Na Abraham Ntambara, Dar es Salaam

CHUO Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT) kimetangaza kurejesha rasmi programu ya maandalizi (foundation programme) baada ya kufanyiwa marekebisho kama ilivyoelekezwa na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TVV).

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Elifas Bisanda, amesema lengo kuu la programu hiyo ni kuwaongezea uwezo wanafunzi waliopungukiwa kwa kiasi kidogo, sifa za kujiunga katika vyuo vikuu nchini kwa vigezo vilivyowekwa na TVV.

“Wanafunzi wanaodahiliwa katika program hii pia wanapata fursa ya kuelewa mbinu mpya za kujifunza kwa njia ya masafa, hususani matumizi ya TEHAMA katika kujifunza,” amesema Profesa Pisanda.

Amesema watakaobahatika kujiunga na masomo ya shahada kwa njia ya masafa kupitia chuo hicho watakuwa wameandaliwa vyema kufuata mfumo huo ambao ni wakisasa zaidi katika kupata elimu ya juu.

 Itakumbukwa kwamba mwezi Julai 2016, TVV ilitangaza kusitishwa kwa programu zote za maandalizi (foundation Programmes) zilizokuwa zinatolewa na vyuo mbali mbali.

“Ni kweli kwamba kulikuwa na programu nyingine ambazo hazikuwa na ubora wa kutosha kuwaandaa wanafunzi kuingia katika masomo ya shahada. Kwa bahati mbaya programu zote zilisitishwa ikiwemo ile ya CKHT, licha ya ukweli kuwa programu ya maandalizi ni muhimu kwa chuo Kikuu huria,” amesema.

Profesa Bisanda ameeleza kuwa kuanzia mwishoni mwa mwaka 2016, chuo hicho kiliendelea kufanya majadiliano na TVV ambapo CKHT kilielekezwa kufanya maboresho katika mtaala na muundo wa programu yake ya maandalizi.

Amesema chuo kilifanya maboresho yaliyotakiwa, yaliyopelekea  TVV kutoa ithibati ya programu hiyo mpya.

Aidha kufuatia maboresho hayo, wahitimu wa programu hiyo watakaofaulu kwa vigezo vilivyowekwa wataruhusiwa kujiunga na shahada ya kwanza katika chuo kikuu chochote nchini.

Ameeleza kwamb programu hiyo ya mwaka mmoja inalenga kuwadahili wenye sifa zifuatazo, wahitimu wa kidato cha sita wenye ufaulu wa angalau pointi 1.5 katika masomo mawili.

Nyingine ni wahitimu wa stashahada kutoka vyuo vinavyotambuliwa na serikali wenye ufaulu wa GPA ya kuanzia 2.0 na wahitimu wa ‘NTA level 5/professionsl Technical Level II Certificate’.

Profesa Bisanda amesena maombi ya kujiunga na programu ya maandalizi yalianza kupokelewa tangu Aprili 10, 2018 na udahili unaendelea hadi Agosti 31, 2018 katika vituo vyote vya chuo hicho vilivyopo Tanzania Bara, Unguja na Pemba.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search