'KIKAO KAZI'

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
tarehe 28 Machi, 2017 alikutana na Mawaziri wa Nishati na Madini wa Serikali za
Tanzania na Uganda Ikulu, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili Maendeleo
ya Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima Nchini
Uganda hadi Chongoleani, Tanga - Tanzania, hususan katika masuala ya kikodi
yatakayotumika katika mradi huo.
Mawaziri hao ni pamoja na Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini
Nchini Uganda, Mhandisi Irene Muloni pamoja na ujumbe wake na Waziri wa Nishati
na Madini Nchini Tanzania Profesa Sospeter Muhongo pamoja na wataalam
kutoka Serikali zote mbili.
Wajumbe wengine ni pamoja na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Mhe. John Lukuvi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Mcheche Masaju
pamoja na Makampuni ya Uwekezaji ya Mkondo wa Juu wa Ziwa Albert Nchini Uganda
ya TOTAL, CNOOC na TULLOW.
Masuala ya kikodi ni moja ya vipengele muhimu katika ukamilishwaji wa
mkataba wa kimataifa kati ya nchi ya Tanzania na Uganda.
Mbali na kukaribisha washiriki wa mkutano huo, Mhe. Dkt. Magufuli
alisisitiza ahadi yake na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni ya
kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati.
Aidha, Dkt. Magufuli aliagiza wawekezaji kutekeleza mradi huo bila
kuchelewa kwa maana Serikali imeshaweka mazingira mazuri ya
utekelezaji wa mradi ikiwa ni pamoja na masuala ya usalama, upatikanaji wa
ardhi, kodi hivyo kupunguza gharama za ujenzi Tanzania.
Pamoja na mambo mengine mawaziri, maafisa na wataalam wa pande zote
husika walikaa na kukubaliana kwamba, rasimu ya makubaliano rasmi ya kuanza kwa
mradi yawe yamekamilika na kuwa tayari katika kipindi cha wiki mbili ili
kuwezesha Marais wa Tanzania na Uganda, kuweka jiwe la msingi kuashiria
ujenzi wa kihistoria wa mradi huo wa bomba la mafuta kutoka Hoima Nchini
Uganda hadi Chongoleani, Tanga-Tanzania.
Mradi huu upo katika hatua ya awali ya tahmini ya mazingira pamoja na
kubaini maeneo mradi utakapopita ili mradi kuweza kutekelezwa kwa kasi pindi
utakapoanza.
Imetolewa na:-
Kitengo cha Mawasilino Serikalini
Wizara ya Nishati na Madini
Machi 29, 2017
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akifungua kikao cha pamoja cha Mawaziri wa Serikali za Tanzania na Uganda
pamoja na wadau kuzungumzia mradi wa ujenzi wa Bomba la Kusafirishia Mafuta
Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga. PICHA NA IKULU
No comments:
Post a Comment