AFYA YAKO: Unayopaswa kufahamu kuhusu Ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB).. #share

Namna ya kumtambua mtu anayeugua ugonjwa wa TB

 Moja ya chanjo muhimu za mwanzo kabisa nilizotaja ni chanjo ya kuzuia ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB). Huu ni ugonjwa hatari ambao unaweza ukamuathiri mtu wa jinsi na rika lolote.
Ugonjwa wa kifua kikuu ni ugonjwa wa kuambukizwa unaosababishwa na aina mbalimbali za vimelea vya bakteria ambao hujulikana kama Mycobacterium tuberculosis. Kifua kikuu ni ugonjwa unaoathiri mapafu, lakini pia ugonjwa huu unaweza  kuathiri sehemu nyingine za mwili pia.
Maambukizi
Kifua kikuu husambazwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kwa njia ya hewa, hasa wakati mtu mwenye maambukizi anapokohoa au kupiga chafya.
Watu wengi wanaishi na vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu bila kuwa na dalili zozote kwa miaka mingi, maambukizi ya aina hii huwa hayana madhara. Lakini baadhi ya watu huweza kupata dalil za kifua kikuu kama kinga ya mwili itapungua.

Watoto wadogo na wazee ni makundi ya watu ambayo hupata maambukizi kirahisi zaidi, hii ni kwasababu kinga ya mwili katika makundi haya ya watu huwa si ya kutosha.

Watu wengine walio katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa wa kifua kikuu ni wale ambao wana magonjwa yanayosababisha upungufu wa kinga mwilini kama vile Ukimwi na magonjwa ya saratani.

Ikumbukwe kuwa watoto hupata maambukizi ya kifua kikuu kwa urahisi sana pale wanapokua karibu na mtu mzima mwenye maambukizi ya ugonjwa huu.
Dailili zake
Dalili za ugonjwa wa kifua kikuu ni pamoja na kukohoa kwa muda wa wiki mbili mfululizo au zaidi, homa za mara kwa mara, kutokwa na jasho jingi hasa nyakati za usiku, kukohoa makohozi yenye damu na kupungua uzito.

Baadhi ya dalili hizi zinaweza zisionekane kwa uwazi hasa kwa watoto, hivyo ni muhimu kuhakikisha kama mtoto anaedhaniwa kuwa na kifua kikuu alishawahi kuishi karibu na mtu mzima ambaye amegundulika kuugua ugonjwa huo katoka kipindi husika.

Vipimo na Jinsi ya kuutambua
Njia ya kwanza ya kutambua kama mtu ana maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu ni kwa dalili alizonazo. Ni muhimu sana kwa daktari kupata maelezo toka kwa mgonjwa kwa umakini mkubwa ili kuona kama mgonjwa ana dalili za kifua kikuu.

Njia ya kitaalamu ya utambuzi wa kifua kikuu ni kwa kutumia X-Ray ya kifua. Pia wataalamu wa maabara hutumia darubini na kufanya uchunguzi wa vimelea maradhi kutoka katika makohozi na aina mbalimbali za majimaji ya mwilini.  

Kipimo cha ngozi kijulikanacho kama TST au Mantoux hutumika zaidi kwa waoto wadogo. Vipo pia vipimo vya damu na vingine vingi vya kisasa vya kijenetiki.  Katika siku za hivi karibuni, aina fulani ya panya waliofundishwa wamekua wakitumika kutambua kama makohozi yana vimelea vya kifua kikuu.
Matibabu na jinsi ya kuzuia
Ugonjwa wa kifua kikuu unatibika na ni muhimu kama mtu ana dalili tajwa awahi katika kituo cha afya kwaajili ya matibabu. Baada ya kuhakikisha kwamba mgonjwa ana kifua kikuu, daktari humuanzishia dawa mgonjwa na kumpa maelezo kuhusu umuhimu wa kumeza dawa kwa wakati.

Ni muhimu kuhakikisha kwamba watoto wote waliozaliwa wanaoata chanjo ya kuzuia maambukizi ya kifua kikuu. Endapo umegundulika kuwa na kifua kikuu, kumbuka kufunika mdomo na pua unapokohoa na kupiga chafya na kutokutema mate hovyo ili usiwaambukize watu wengine.

Ni muhimu uwafahamishe ndugu na marafiki kwamba unaugua kifua kikuu na upo kwenye matibabu ambayo pia ni lazima yakamilike ili kuzuia hatari ya kupata kifua kikuu kilicho sugu ambacho matibabu yake ni magumu sana.


Kwa mtu mwenye kifua kikuu ni muhimu kupata ushauri nasaha kwa ajili ya kupima virusi vya ukimwi (VVU) kwa sababu magonjwa haya yana uhusiano wa karibu.

Makala hii imeandaliwa na Dk. Pius Muzzazzi

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search