Ukame na Uharibifu wa Mazingira kutokana na ongezeko la mifugo katika vyanzo vya maji umesababisha kukauka kwa Bwawa tegemeo la Itaswi.. #share
Bwawa la Itaswi ambalo ni tegemeo la upatikanaji wa maji kwa wananchi wa vijiji zaidi ya 20 katika wilaya ya kondoa mkoani dodoma limekauka hali ambayo imewafanya wananchi wengi kutumia maji kutoka kwenye makorongo na visima vifupi vinavyochimbwa katika kingo za bwawa hilo ambayo siyo safi na salama.
Wananchi wa vijiji mbalimbali vinavyotegemea maji kutoka bwawa hilo la Itaswi maarufu kwa jina la bwawa la Kisaki lililojengwa mwaka 1959 wamesema bwawa hilo ambalo pia ni chanzo muhimu cha maji cha mto Tarangire na uhai wa hifadhi ya taifa ya Tarangire limewahi kukauka mwaka 1994.
Baadhi ya sababu zinazotajwa kusababisha kukauka kwa bwawa hilo ni ukame na uharibifu wa mazingira na ongezeko la mifugo inayochunga kwenye vyanzo vya maji ikiwemo katika pori la akiba la Mkungunero.
Baadhi ya akina mama waliokutwa wanachota maji kwenye visima vifupi vya kienyeji vilivyochimbwa kwenye kandokando ya bwawa hilo akiwemo Bi Amina Salehe wamesema maji wanalazimika kutumia maji hayo kwasababu hawana njia nyingine ya kupata maji safi na salama.
Nae mkazi mwingine wa Itaswi, Ramadhan Kanuti amesema bwawa hilo la Itaswi limejaa tope na hivyo linahitaji kusafishwa na kutoa tope ili kuongeza kina na kufanya maji yanatakayoingia bwawani yaweze kutumika kwa muda mrefu.
“Tunawaomba wenzetu wa pori la akiba la Mkungunero watusaidie kukabiliana na changamoto hii ambayo inawaathiri wananchi wengi maana kama unavyoona akina mama wanahangaika kutafuta maji kwenye makonrogo” alisema Ramadhan Kanuti.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Itaswi wilayani kondoa Saidi Mohamed Chobu ameiomba serikali na wadau kusaidia kulikarabati bwawa la Itaswi na kuondoa tope ili kuwaondolea wananchi adha ya kuchota maji kwenye madimbwi na makorongo ambayo maji yake siyo safi na salama.
Alisema hata mwaka 2004 wakati Bwawa hilo lilipobomoka, Hifadhi ya Tarangire ndiyo iliyotoa msaada wa ukarabati kwasababu inatambua umuhimu wa bwawa hilo kwa wananchi na mifugo.
“Hawa wenzetu wa hifadhi ya taifa ya Tarangire wanafahamu kwamba bwawa hilo ni chanzo muhimu muhimu cha maji ya mto Tarangire na wanyamapori kwenye hifadhi hiyo kwahiyo waliuona umuhimu huo na tunaomba watambue kwamba wananchi wetu bado wana uhitaji mkubwa wa msaada” alisema diwani Said Mohamed Chobu.
Alipoulizwa kuhusu maombi ya wananchi hao Meneja wa pori la akiba la Mkungunero, Emmanuel Bilaso amewataka wananchi kuwasilisha maombi yao kwa maandishi na yeye atawasilisha makao makuu ya Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania Tawa ili yaweze kufanyiwa kazi.
“Kwakweli kwa jinsi nilivyoliona hili Bwawa la Itaswi naona kuna umuhimu wa kusaidia kulikarabati, kwani tukifanya hivyo tutasaidia kupunguza presha ya mifugo inayoingia kwenye pori letu la Mkungunero kutafuta maji na kuathiri uhifadhi: alisema Emmanue Bilaso.
Kwa upande wake Meneja wa mawasilaiano wa mamlaka ya wanayamapori Tanzania TAWA, Twaha Twaibu alisema mamlaka hiyo imekuwa na utamaduni wa kusaidia miradi ya kijamii kwenye vijiji vinavyozunguka mapori ili kujenga mahusiano kati ya jamii na mapori ya akiba.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kondoa Mwalimu Fares Kibasa amesema serikali inatambua tatizo la kukauka kwa bwawa la Itaswi na kwamba tayari juhudi za kuchimba visima katika vijiji kuzunguka bwawa hilo zinaendelea.
Mwalimu Kibasa alisema halmashauri imepanga kuchimba visima zaidi ya 15 kwenye vijiji mbalimbali kuzunguka bwawa hilo na kwamba mipango ya muda mrefu inayohamasishwa kwa wananchi ni kupanda miti kuzunguka bwawa hilo na kutilia mkazo uhifadhi wa mazingira kwenye vyanzo vya maji.
“Kukauka kwa bwawa la Itaswi ni changamoto kubwa kwa wananchi wengi na tayari juhudi za kuchimba visima virefu katika vijiji kuzunguka bwawa hilo zinaendelea kwani wilaya ya kondoa haina mito ya maji yanayotirika mwaka mzima, kwahiyo suluhisho la maji Kondoa ni visima” alisema mwalimu Fares Kibasa, Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya wilaya ya Kondoa.






No comments:
Post a Comment