Mashtaka 23 yanayomkabili mhasibu Takukuru yagonga mwamba...soma habari kamili na matukio360..#share
Na Abdulrahim Sadiki
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi
Kisutu imetupilia mbali maombi ya upande wa utetezi katika kesi ya utakatishaji
fedha na kumiliki mali za bilioni 3.6 kinyume na mshahara inayomkabili aliyekuwa
mhasibu wa Takukuru, Godfrey Gugai.
Maombi ya upande wa utetezi
yalilenga kuiomba mahakama hiyo kuyaondoa mashtaka 23 ya utakatishaji fedha
yanayomkabili Gugai na wenzake.
Uamuzi wa kuyatupa maombi
hayo umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya Wakili wa serikali,
Peter Vitalis kusema shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya uamuzi.
Hakimu Simba amesema
mahakama hiyo inatupilia mbali maombi ya utetezi kwa madai mashtaka 23 ya
utakatishaji fedha yapo kimakosa katika hati ya mashtaka.
"Hati ya mashtaka ipo
sahihi, hivyo natupilia mbali maombi hayo na upande wa Jamhuri unaweza kuendelea
na hatua za upelelezi,".
Baada ya kusema hayo aliahirisha
kesi hiyo hadi Desemba 28,2017.
Mbali ya Gugai, washtakiwa wengine ni George
Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa 43, kati ya hayo
19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi
kipato halali.
Gugai anakabiliwa na kosa la kumiliki mali kinyume na
kipato chake, ambapo alitenda kosa hilo kati ya Januari 2005 na Desemba 2015.
Inadaiwa akiwa jijini Dar es Salaam kama mwajiriwa wa
Takukuru alikuwa akimiliki mali za zaidi ya bilioni 3.6 ambazo hazilingani na
kipato chake cha awali na cha sasa cha zaidi ya milioni 800, huku akishindwa
kuzitolea maelezo.
No comments:
Post a Comment