Chadema waituhumu CCM kucheza rafu uchaguzi Kinondoni...soma habari kamili na matukio360...#share

Na Abraham Ntambara, Dar es Salaam

CHAMA cha Chadema kimedai kuwa  baadhi ya viongozi wa CCM Kinondoni wanapita nyumba kwa nyumba kununua na kuandika namba za shahada za kupigia kura za wananchi na kuwadanganya hazitatumika na  watapewa nyingine.

Pia kimemtuhumu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuwa anafanya hujuma za kutaka kuibeba CCM ili ishinde katika uchaguzi wa marudio ya Ubunge wa Februari 19,2018.
Mkuu wa Operesheni wa Uchaguzi Chadema Benson Kigaila akizungumza na waandishi wa habari juu ya mwenendo wa uchaguzi mdogo wa ubunge Kinondoni.

Kufuatia vitendo hivyo kitaandika barua ya malalamiko  kwenda Tume ya Taifa ya Uchaguzi  (NEC) kuhusu njama hizo.

Kimetoa tuhuma hizo leo jijini Dar es salaam katika mkutano wake na waandishi wa habari kuelezea mwenendo mzima wa uchaguzi Jimbo la Kinondoni na kuwa wanamshutumu Mkurugenzi wa halmashauri ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli kwa kuiandikia Chadema barua mbili ikilalamikiwa kuvunja kanuni za maadili ya uchaguzi katika kampeni zao.

Mkuu wa Operesheni ya Uchaguzi wa Chadema Benson Kigaila amesema katika barua ya kwanza wanalalamikiwa na mtu asiyejulikana kuwa Januari 28, 2018 walifanya kampeni ya nyumba kwa nyumba na maandamano nje ya muda uliopangwa enrollment la  Kigogo kuanzia Mbuyuni mpaka Baa ya Londor badala ya Ndugumbi Mikoroshini.

“Na katika barua ya pili tunalalamikiwa na chama cha CUF Lipumba, kuwa  tunatumia salamu za CUF kwenye jukwaa letu, tunaweka bendera ya CUF katika jukwaa letu, viongozi wa CUF kukaa katika meza kuu ya viongozi na kupanda katika jukwaa letu na kuwatumia viongozi wa CUF kupita nyumba hadi nyumba wakiomba kura huku wakiwa wamevaa sare za CUF,” amesema Kigaila.

Kigaila amedai tuhuma hizo ni za kutengenezwa  za uongo na kwamba kama ni kampeni walifanya kweli Kigogo kama ratiba ilivyokuwa inasema na hawakutakiwa kuwa Ndugumbi kama inavyodaiwa.

“CCM hawachaguliki kinondoni, walishalikoroga kwa kumteua Maulid Mtulia aliyeukana ubunge, wanakinondoni wameshachukia hilo, hivyo haya ni maelekezo ambayo wakurugenzi walipewa kuhakikisha CCM inashinda,” amesema Kigaila.

Katika hatua nyingine kampeni meneja wa Salum Mwalimu, Said Kubenea amesema mkurugenzi huyo amekuwa akiwachezea kwani alishawahi kufanya hivyo katika uchaguzi wa Meya wa Kinondoni na kuapa kuwa hawatakubali tena kuchezewa.

Kwa upande mwingine Kubenea amedai kuwa CCM inapita nyumba kwa nyumba kununua na kuandika namba za shahada za kupigia kura kwa wananchi wakiwadanganya kuwa hazitatumika na  watapewa nyingine.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kutaka kupunguza idadi ya kura ili waweze kupenyeza kura zao siku ya uchaguzi.

Hivyo amewataka kuacha mara moja kufanya hivyo kwani wakiendelea watatuma vijana wao kwa ajili ya kulifuatilia jambo hilo ili kulizuia.




About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search